Ripoti ya Utafiti wa TAMWA 2012 kuhusu Ukatili wa Kijinsia katika Jamii Tanzania Bara

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakisikiliza taarifa ya utafiti huo

RIPOTI YA UTAFITI WA TAMWA KUHUSU UNYANYASAJI WA KIJINSIA

1.0 UTANGULIZI
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), katika mpango mkakati wake wa miaka mitano 2000-2014, pamoja na mambo mengine kimepanga kufanya shughuli ambazo zitaimarisha elimu kwa mtoto wa kike kwa kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa vile vinavyoathiri wanawake na watoto. Vitendo hivyo ni pamoja na ubakaji, kulazimisha watoto wa kike kukatisha masomo na kuolewa, ukeketaji na familia kutelekeza watoto ambavyo kwa pamoja vinamnyima mtoto wa kike haki yake ya msingi ya kupata elimu. Kwa sababu hiyo, baada ya utafiti uliofanyika Februari 2012 katika shule za sekondari za kata kwenye mikoa 20 nchini kuchunguza mambo yanayochangia wanafunzi kukatisha masomo hasa kwa ujauzito na wengi kufeli mitihani ya taifa, mwezi Aprili 2012 TAMWA imefanya utafiti mwingine wa kihabari (journalistic survey) mwingine katika mikoa 20 ikiwepo 15 ya Tanzania Bara na Mitano ya Zanzibar kuhusu hali ya vitendo vya ukatili nchini. Vitendo vilivyolengwa ni ubakaji, vipigo kwa wanawake, kutelekeza wanawake na watoto, ukeketaji na kulazimisha watoto wa kike kulazimishwa kukatisha masomo na kuolewa.
TAMWA imepata msukumo wa kufanya utafiti huu wa kihabari kutokana na ukweli kwamba matendo haya ya kikatili yameshamiri s nchini, na hakuna utafiti wa hivi karibuni ambao ungesaidia vyombo husika kupima kiwango halisi cha matendo na matukio haya. Taarifa zilizokuwapo hadi utafiti huu unafanyika, kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa wa mwaka 2010, ni kwamba zaidi ya asilimia 39 ya wanawake nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili tangu wakiwa na umri wa miaka 15. Watuhumiwa wa unyanyasaji huu kwa kiwango kikubwa ni wanaume. Ripoti ya Polisi Zanzibar inasema katika mwaka 2011, yalikuwapo matukio 268 ya unyanyasaji yaliyoripotiwa; lakini kesi zilizofikishwa mahakamani ni 55 tu. Katika zote hizo, kesi moja ndiyo iliyomtia mtuhumiwa hatiani.
Kutokana na hali hii, na kwa kuzingatia mkinzano wa kisheria kati ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 juu ya umri wa mtoto kuolewa, na adhabu anayostahili, TAMWA imefanya utafiti kuona jinsi ya kupunguza ukatili wa wanawake kupitia habari za ushahidi wa matendo hayo na kupendekeza suluhisho muafaka. Lengo kuu la utafiti huu limekuwa ni kukusanya taarifa za awali zinazoonyesha halisi ya ubakaji, watoto wa kike wanafunzi kulazimishwa kuolewa, ukeketaji, vipigo kwa wanawake na watoto na wanawake kutelekezwa ili kujenga msingi wa kisayansi juu ya chanzo cha ukatili huo na kutafutua ufumbuzi.
2.0 WILAYA ZA UTAFITI
Utafiti huu ulifanyika katika wilaya moja kila mkoa wenye mikoa 20 ambayo ni: Morogoro (Mvomero), Mtwara (Newala), Shinyanga (Kahama), Dar es Salaam (Ilala, Temeke na Kinondoni), Kilimanjaro, (Same), Pwani (Mkuranga) Mara (Tarime), Manyara (Simanjiro),Tanga (Handeni), Kigoma (Kasulu), Iringa (Kilolo), Mbeya (Rungwe) Singida (Iramba), Dodoma (Kondoa ), Arusha (Karatu) na Njombe (Njombe). Mikoa ya Zanzibar na wilaya zake kwenye mabano ni Kaskazini Pemba, (Micheweni na Wete), Kusini Pemba (chakechake) Kaskazini Unguja (Kaskazini A, Kaskazini B), Kusini Unguja (Kusini Unguja), Mjini Magharibi (Wilaya ya kati). Hata hivyo ripoti hii inatokana na taarifa za wilaya 15 za Tanzania Bara. Ripoti ya Tanzania Visiwani imeandaliwa na ofisi ya TAMWA na TAMWA Zanzibar itazinduliwa huko Zanzibar.
3.0 WATAFITI NA MBINU ZA UTAFITI
TAMWA iliandaa dodoso ambalo liliwaongoza wanahabari watafiti katika kukusanya taarifa; kikaandaliwa kikao kifupi cha kuwaandaa wanahabari hao, na kila mshiriki akapewa nakala ya dodoso. Baadaye wanahabari walipewa barua za utambulisho ili kuwarahisishia utambulisho katika maeneo ya kazi, na kila mtafiti alishauriwa kuchagua kata tatu katika wilaya alikotumwa, na akashauriwa afanya utafiti wake katika vijiji vitatu – kimoja kutoka kila kata. Kwa kuwa ulikuwa utafiti wa kihabari, wahusika walishauriwa kutumia mbinu za kihabari kupata taarifa zao. Vyombo vya habari ambavyo TAMWA ilivishirikisha katika kufanya utafiti huu ni Tanzania Daima, Mwananchi, Jamhuri, The Guardian, ITV, The Citizen, Daily News, Nipashe, Majira, Habari Leo, The African, Mtanzania, Uhuru, The Habari.com, Dira, na TAMWA.
4.0 MAENEO YALIYOTAFITIWA
Utafiti huu uliweka kipaumbele katika maeneo matano ambayo ni: ubakaji, wanafunzi kulazimishwa kuolewa, wanawake kupigwa, wanawake na watoto kutelekezwa, na ukeketaji. Kwa kila eneo, utafiti ulilenga kuibua chanzo, ukubwa, athari, na pendekezo la ufumbuzi wa tatizo.
5.0 CHANGAMOTO ZA UTAFITI
Miongoni mwa changamoto zilizowakabili watafiti ni woga wa wahusika katika kuzungumzia unyanyasaji. Baadhi yao walidhani kwamba taarifa zinazowahusu zikitolewa kwenye vyombo vya habari zingeweza kusababisha wao kudhurika au kushitakiwa. Katika baadhi ya maeneo, miundo mbinu ilikuwa mibovu na kusababisha watafiti kuchelewa kufika na kuanza kazi mapema. Urasimu wa baadhi ya viongozi ulichangia kukwamisha upatikanaji wa takwimu katika maeneo kadhaa. Baadhi ya wahojiwa walitaka walipwe kabla hawajatoa taarifa walizonazo.
6.0 MATOKEO YA UTAFITI
Kijumla, matokeo kutoka mikoa mbalimbali yameonyesha kwamba ukatili wa kijinsia ni moja ya matatizo ya msingi katika jamii yetu. Sababu na mazingira ya ukatili huo yanashahabiana kwa sehemu kubwa; na baadhi ya mapendekezo yanafanana. Kilicho dhahiri ni kwamba mkinzano wa kisheria kuhusu umri wa mtoto kuolewa, na mila na desturi za baadhi ya makabila katika mikoa husika, ni mambo yanayochangia kushamiri kwa matukio ya unyanyasaji huu wa kijinsia.
6.1 UBAKAJI
Dhana ya ubakaji ni pana kijamii na kisheria. Kijamii, ubakaji katika maeneo mengi umeelezwa kama ngono ya kulazimisha; lakini kisheria, ni pamoja na kufanya ngono na mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18, hata kama amekubali. Kwa sababu hiyo, taarifa juu ya ubakaji zipo nyingi vijijini, hasa katika maeneo ambayo watoto huolewa wakiwa chini ya miaka 18. Katika baadhi ya mikoa, yamedhihirika matukio ya ubakaji ambayo husababishwa na mabavu ya baadhi ya wanaume, ulevi, matumizi mabaya ya kipato, malezi duni, ushirikina, umaskini wa wasichana na wazazi wao, na tamaa mbaya ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye aibu wasioweza kujadiliana na wanawake kuhusu taama yao hiyo. Kimsingi, ubakaji ni tatizo la kitaifa; na moja ya njia za kulipunguza ni kubadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ili kuzuia wanaume kuoa watoto wa kike walio chini ya miaka 18. Lakini kingine kikubwa kilichojitokeza na ambacho kinahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ni kwamba wahusika wengi wa ubakaji hawafikishwi mahakamani na wale wanaofikishwa mahakamani wanaachiwa huru kutokana na vyombo vya kutoa haki kugubikwa na rushwa na kukosekana kwa ushahidi kutokana na wananchi kutokujua jinsia ya kutunza ushahidi wa ubakaji. Ili ushahidi wa ubakaji uwe dhahiri, mtu aliyebakwa anapaswa asioge wala kubadilisha nguo alizokuwa amevaa wakati anabakwa na anatakiwa kuwahishwa polisi kupata PF3 na kisha kwenda hospitali kupimwa kupata ushahidi na kupatiwa dawa tiba na kuzuia maambukizi ya magonjwa hatari kama vile virusi vya UKIMWI. Lakini pia kuna unyanyapaa mkubwa kwenye jamii kuhusu suala zima la ubakaji. Jamii bado inauonea haya uovu huu ambao unachangia kwa kiasi kikubwa mimba mashuleni na maambukizi ya virusi vya UKIMWA.
6.1.1 Visa Mkasa:
(a) Katika Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, yapo matukio ya wanaume kufanya ngono na watoto wadogo, lakini hatua kali hazichukuliwi. Upo mfano wa mtoto mdogo wa miaka 10 aliyetoroshwa na kijana, akaacha shule. Ofisa Mtendaji alipoletewa taarifa hizo alimchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitali, hatimaye polisi wakaanza kumsaka mtuhumiwa. Lakini mtoto amekataa katakata kurudi shuleni. Tatizo kubwa ni kwamba wazazi wengi hawako tayari kufikisha masuala haya polisi, na hata wanaposaidiwa kufanya hivyo, wasichana na wazazi hawapatii polisi ushirikiano. Watuhumiwa wengi huachiwa huru.
(b) Hali ni ile ile katika Wilaya ya Njombe, Mkoa wa Njombe, ambako usiri wa jamii kuhusu matukio haya umefanya mengi yapite bila kuripotiwa; huku baadhi ya watendaji wakikana kabisa kuwapo kwa matukio hayo. Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya, Sarah Dumba anasema: “Matukio haya hufanyika hata kwa mzazi kumbaka mtoto au mtoto kumbaka mzazi na kwamba matukio haya huripotiwa Polisi na pia hunifikia kwa sababu tunafanya kazi na Polisi kwa ukaribu na ushirikiano ambapo matukio ya ubakaji 37 kuanzia Julai mwaka 2011 hadi Aprili mwaka huu (2012) yalinifikia, pamoja na imani za kishirikina pia wapo wanaobakwa kwa sababu tofauti, hawa wamekuwa wagumu kuripoti polisi na kuja kutoa ushahidi pindi kesi inapofikishwa mahakamani, hivyo mahakama inakosa ushahidi wa dhati wa kumtia mtu hatiani.”
Taarifa za Mahakama ya Wilaya ya Njombe zinaonyesha kuwa kesi 28 za ubakaji zimewahi utolewa uamuzi, na nyingine 28 zinaendelea.
(c) Kuhusu ubakaji usababishwao na ulevi, Alphonce Chaula, Mkazi wa Kijiji cha Mtwango, Kata ya Mtwango, anasema: “Utakuta mwanamke amekaa kilabuni ananunuliwa pombe anakunywa bila kuuliza pombe hiyo ananunuliwa kwa maana gani; akitoka hapo kuelekea kwake mwanaume aliyemnunulia pombe anamvizia na kumbaka. Kesho yake wanasema sababu ni pombe tu yanaishia hivyo. Wanawake wengi hasa ambao hawajaolewa wanabakwa sana, lakini wanaona aibu kuripoti kwani wanahisi kama watajidhalilisha na watakosa waume wa kuwaoa. Cha muhimu hapa ni kuwa wazi tu, kwani mficha maradhi mwisho wa siku kifo humuumbua,”
(d) Mkoani Pwani, Katibu wa Dawati la Jinsia, Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Mkuranga, Pascal Machangu, anasema kwa mwaka 2011 pekee walipokea kesi 18. Miongoni mwa hizo, kesi za ubakaji halisi ni 10; na zinazohusu kuwapa mimba wanafunzi ni kesi nane (8). Kesi tano tayari zimeshatolewa uamuzi; tatu bado zipo mahakamani.
(e) Wilayani Temeke, Dar es Salaam, kuna mtoto aliyebakwa akiwa na umri wa miaka tisa (9) tu. Mzazi wake, Mohammed Nassoro, anasema; “Mtoto wangu Latifa alibakwa mwaka jana akiwa na umri wa miaka 9, kesi ipo mahakamani na mtuhumiwa yupo nje. Kwa kweli kitendo cha mtoto kubakwa kinachangia maambukizi ya Ukimwi. Kwa upande wa mwanangu nashukuru yuko salama.”
(f) Wilayani Kahama, Shinyanga, lipo tukio la mwaka 2011 la mwanaume mfanyabiashara mwenye miaka 40 aliyemnajisi mtoto wa miaka mitano (5).
(g) Katika Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni, madaktari wanasema wanapokea matukio ya ubakaji yasiyopungua matatu (3) kila siku. Waliohojiwa wamesema chanzo ni ulevi wa pombe, uvutaji wa madawa ya kulevya na ahadi zisizotimia kutoka kwa wasichana. Elias Aman Akamwile (57), Mjumbe wa Mtaa Bunju B, Kata Mabwepande, anasema: “Wasichana wanabakwa kwa sababu wanapeana ahadi za mapenzi halafu baadaye wanakataa kutimiza ahadi hiyo, ndipo mwanaume anamvizia ili akufanyie kwa nguvu. Wanaobaka lazima huwa wanalipiza visasi, hawabaki bila sababu.”
Katika kituo cha Polisi cha Wazo Hill, mwaka 2010 ziliripotiwa kesi za ubakaji 71; na miongoni mwa hizo, 24 zilifikishwa mahakamani. Kesi nne (4) ziliamuliwa, 47 zikafutwa. Mwaka 2011 kesi za ubakaji 88 ziliripotiwa polisi; miongoni mwa hizo 32 zilifikishwa mahakamani. Kesi 56 bado ziko katika upelelezi. Mwaka huu 2012, kati ya Januari na Machi, kesi za ubakaji ziizoripotiwa ni 37. Zilizofikishwa mahakamani ni kesi 10; na kesi 27 ziko katika upelelezi.

6.2 WANAFUNZI KULAZIMISHWA KUOLEWA
Wanafunzi kulazimishwa kuolewa nalo ni tatizo la kitaifa ambalo limejitokeza katika mikoa yote. Wengi wao huolewa wakiwa na umri wa miaka 12 hadi 16. Sababu kubwa zinazotajwa ni umaskini wa wazazi, watoto kushindwa shule, ujauzito, tamaa za wanafunzi wenyewe, na migogoro ya kifamilia.
6.2.1 Visa Mikasa
(a) Veice Ngwada (32), Muuguzi katika Hospitali ya Mbweni, kitengo cha kuzalisha, Kata Mbweni, Kinondoni, Dar es Salaam, anasema baadhi ya watoto wanaozalia pale wana umri wa miaka 14 hadi 18. Mwaka 2010 walikuwa 18 watoto wajawazito 52 wenye umri wa miaka 15-18. Mwaka 2011 watoto wajawazito 20 walikuwa na umri wa miaka 14 hadi 17; waliokuwa na miaka 18 walikuwa watoto 22.
(b) Sharifa Rashid (14), Kidato cha Kwanza, Shule ya Sekondari Mabwe, anasema: “Nilisoma na rafiki yangu la kwanza hadi la nne akaja akafeli. Aliacha shule akiwa darasa la nne; alishindwa mtihani kwa kuwa alikuwa mtoro, ataniambia anataka kuolewa. Nafikiri kwa sababu aliishia darasa la nne anaona akiolewa atapata faida kwa mumewe. Wazazi wanaona anaweza akapata mimba ambayo haina baba, hivyo wanaona ni bora wamuozeshe ili azae kwa mume kuliko kubebea mimba nyumbani.”
(c) Katika baadhi ya shule mkoani Pwani, walimu wamekuwa wakigombana na wazazi ambao hawataki watoto wao wafaulu kwenda sekondari, kwa kuhofia kwamba akiendelea na masomo atachelewa kuolewa. Ofisa Elimu wa Wilaya ya Mkuranga anasema mwaka 2011 kulikuwa wanafunzi 15 wa sekondari waliripotiwa kuwa na mimba, na hivyo kukatisha masomo; watatu walifikishwa polisi, watatu mahakamani; na mmoja kwa mtendaji kata. Wazazi wa watoto wanane (8) hawakuchukua hatua yoyote.
(d) Mkurugenzi wa Mtendaji wa Wilaya ya Kahama Eliza Bwana anasema ndoa za kulazimisha watoto ni nyingi katika eneo lake kutokana na mila na desturi za wakazi wa eneo hilo. Baadhi yao huwatoa watoto shuleni na kuwaoza kwa wanaume wasio chaguo lao, kwa vile wanakuwa wameshapokea mahari kisirisiri. Kwa sababu hiyo, wazazi kama hao hulazimisha watoto wao wafeli mtihani wa darasa la saba ili waolewe. Anasema mtoto wa shule ambaye wazazi wake wameshapokea mahari hufikia mahali wazazi wake wanamuita “mtoto wa watu” kwa maana kwamba ni mke wa mtu! Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa Wilaya, Jacqueline Ntulo, wasichana katika jamii hiyo hutazamwa kama mtaji; na masahibu haya huwapata watoto wenye umri mdogo kuanzia miaka 12 na 13.
(e) Ndoa nyingine za umri mdogo huchangiwa na mazingira magumu ya shule, ukiwamo umbali kutoka nyumbani hadi shuleni. Wilayani Mvomero, Morogoro, Mtendaji wa Kata ya Kanga, Buhatwe Matage, anasema wasichana hupata mimba na kuolewa kutokana na wazazi kushindwa gharama za kulipia elmu yao, lakini pia wapo wanaoathiriwa na umbali.
Anasema: “Umbali wa shule unaosababisha watoto kuamua kuolewa kuepuka mateso ya mwendo wa kasi na kushinda na njaa kwa siku nzima kutokana na kukosekana kwa chakula shuleni hivyo jamii inatakiwa kupewa elimu ya umuhimu wa kupata elimu kwa jamii nzima, ujenzi wa mabweni katika Sekondari za kata na Uchagiaji wa chakula kwa wazazi ili watoto wapate lishe.” Baadhi yao hutembea kilomita 10 hadi 20 kila siku, wakikumbana na uchovu, njaa na vishawishi vingi njiani.
(f) Mzazi mmoja kutoka Iramba, Singida, Joyce Lufega, mkazi wa Kijiji cha Lunsanga, katika Kata ya Mtenkente ward, anakiri kwamba alimshawishi binti yake aolewe mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, ili apate mahari ya shilingi 100,000/-. Anasema: “Nilimlazimisha binti yangu aolewe, lakini ndoa yenyewe ilidumu kwa miaka minne tu, kwa sababu msichana alikuwa bado mchanga mno hajastahili kuhimili majukumu ya kifamilia.”
(g) Mwathirika mwingine wa uamuzi wa wazazi kumharibia shule ili aolewe, ni Grace Ezekiel (26), mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri. Anasema mara alipohitimu elimu ya msingi, alinyimwa fursa ya kuendelea na sekondari mwaka 2002: “Nilikaa nyumbani kwa miaka mitatu, baadaye nikalazimishwa niolewe mwaka 2006. Wazazi wangu walipokea mahari ya shilingi 200,000/-.”
(h) Katika Wilaya ya Karatu, Manyara takwimu zinaonyesha kwamba katika Kata ya Endamarariek mwaka 2012 pekee, wanafunzi wa kike 14 wameripotiwa kupata mimba katika serikali za shule za kutwa. Mtendaji wa Kata ya Endamarariek, Omari Mshana, anasema: “Changamoto kubwa tunayokumbana nayo ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wanafunzi na wazazi wenyewe. Inatuwia vigumu kuwachukulia hatua wahusika kwani mara nyingi mabinti hawa huhamishiwa sehemu nyingine mara tu anapopata mimba. Mara nyingi wanafunzi hawa hushurutishwa na wazazi wao kutowataja wanaume waliowapatia mimba na hivyo kudanganya kwamba wamepatiwa mimba wakiwa safari na watu wasiowajua.”
Naye Mtendaji wa Kata ya Rhotia, Jackson Sulle, anasema: “Tumepokea kesi saba za mabinti waliopewa mimba mwaka huu lakini wote wametoroshwa kupelekwa sehemu zisizofahamika.”
(h) Katika Wilaya ya Simanjiro, yapo matukio ambayo hutokanana watoto wenyewe kujiachia wapate mimba ili wafukuzwe shule. Ofisa Elimu ya Msingi wa Wilaya, Jackison Mbise, anasema kuachishwa shule kuna sura ya mimba na utoro: “Unaweza kukuta kati ya wanafunzi 194 wanaoanza shule, wanakuja kumaliza kati ya 40, 70 ama 100, wengine wanatoweka kwa njia kama hizi, wengi wa hawa wanaoacha shule ni wasichana, ingawa na wanaume kwa uchache wapo na wao huenda kuchunga Ng’ombe.”
7.0 UKEKETAJI
Ukeketaji uliripotiwa katika maeneo kadhaa, kwa kuwa hii ni mila ya makabila fulani nchini. Katika baadhi ya wilaya, kwa mfano Kilolo, mkoani Iringa, hakuna tatizo la ukeketaji. Katika sehemu nyingi za Jiji la Dar es Salaam, utafiti haukubaini ukeketaji. Hata hivyo, imebainika kuwa ukeketaji upo katika Kata ya Kitunda, kwa sababu wengi wa wakazi wake ni jamii ya watu kutoka Mkoa wa Mara, hasa Wakurya ambao moja ya mila na desturi zao ni kukeketa watoto wa kike. Lakini kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Renatus Ruhungu, ukeketaji umepungua sana kutokana na jitihada za wanaharakati na serikali kuelimisha umma na kuupiga vita.
Vile vile, utafiti umeshindwa kuthibitisha matukio ya ukeketaji katika Wilaya ya Handeni, Tanga; na Rungwe, mkoani Mbeya. Hata hivyo, jamii za mikoa kadhaa bado zinaendelea na mila ya ukeketaji, ingawa kwa kiwango kidogo.
7.1.0 Visa Mikasa
(a) Kuna dalili kwamba kasi ya ukeketaji imepungua katika Wilaya ya Karatu, lakini taarifa zinasema ukeketaji unafanywa kwa siri, kama anavyosema Mratibu wa Kata ya Karatu, Langew Ama: “Ukeketaji hufanywa katika maeneo ya vijijini ambapo watoto wachanga hukeketwa kwa siri pasipo kuwepo na sherehe za kimila ambazo kwa zamani ilikua ni lazima kwa zoezi kama hilo.”
(b) Katika Wilaya ya Kondoa, Dodoma, ukeketaji bado unafanyika lakini kwa kiwango cha chini, kutokana na ushawishi uliofanywa na wanaharakati. Sophia Seleman mkazi wa Kijiji cha Muluwa, Kata ya Suruke, anasema dhana ya ukeketaji ililenga kumfanya mwanamke asiwe na tamaa za kimwili. Anasema: “Siku hizi ni tofauti sana, kwani hapo zamani mwanamke asiyekeketwa alionekana ni malaya pia hakuweza kuheshimiwa wala kuthaminiwa yaani hakuweza kufanya chochote mbele ya wenzake, hata mwanangu amekeketwa. Sherehe za kuwatoa waliokeketwa ni maarufu kama ‘Lofumiavare,’ sherehe hizi zilifanyika wakati wa kuwatoa nje mabinti waliokeketwa, ambapo watu walikula na kunywa pamoja na kucheza, pia baadhi ya mabinti waliolewa kupitia sherehe hizi, na wengine waliambulia kubebeshwa mimba na wanaume wanaohudhuria sherehe hizo kwani hufanyika usiku.” Lakini Mwenyekiti wa Kijiji cha Tugufu, Kata ya Suruke, Yahaya Mohammed, anasema: “Kwa sasa yanafanyika kwa kificho kwani wazazi wanaweza kumuhamisha mtoto wanayetaka kumkeketa kutoka kata moja kwenda nyingine na wengine hudiriki kuwakeketa wakiwa wachanga.”
Hali ni ile ile katika Wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro. Vitendo vya ukeketaji vinafanywa kwa siri sana. Kwa Kipare kukeketa kunaitwa “kutavana;” na Wamasai wanasema “emorata.” Watoto wa kike wakishakua wakubwa, husubiriwa kipindi cha kufunga shule ndipo huchanganywa na watoto wa kiume waliotoka jando na kufanyiwa sherehe ya pamoja kugopa kugundulika kuwa wamekeketa watoto wao. Lakini Mwenyekiti Kijiji Darajani, Tatu Mkumbwa, anasema: “Wanajificha sana. Huwezi kusikia suala la ukeketaji siku hizi, lakini utamgundua mtoto wakati wa sherehe zao. Wanasema mtoto wa kike asipokeketwa hata akifikisha umri wa miaka 30 anaonekana mtoto mbele ya wenzake waliokeketwa, na hawezi kutoa uamuzi au ushauri akasikilizwa. Usipokeketwa huwezi kuingia unyago, kwa hiyo kimila ni lazima ukeketwe; lakini inafanyika kwa siri.”
(c) Wilayani Simanjiro ambakoo asilimia 95 ya wakazi wake ni Wamasai na Waarusha, ukeketaji unaendelea kwa kiwango kikubwa, ingwa wakeketaji wameacha kukeketa wasichana wakubwa (miaka 14-18). Badala yake wanakeketa watoto wadogo wenye umri wa wiki moja hadi mwezi mmoja.
Nang’urutu Kariayi (49), mkazi wa Narokusoito kata ya Langai, ni ngariba maarufu katika eneo hilo ambaye alianza kazi yake hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita. Anasema wanalinda mila zao, lakini wanakwepa kukamatwa. “Kwa siku nakata (nakeketa) hata zaidi ya watoto 10 kwa sababu mtu mmoja anaweza akawa ana mabinti watano; na ile kitu siyo ngumu kwa sababu haina mfupa,” anasema Kariayi.
(d) Moja ya wilaya za mfano ni Iramba, mkoani Singida. Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa wialaya hiyo, Hezron Msule, ukeketaji umekoma tangu mwaka 2005. Anasema mwaka huo ngariba wapatao 50 walikabidhi zama zao za kukuketea, baada ya kazi kubwa za wanaharakati na serikali kupinga ukeketaji na kuelimisha jamii juu ya madhara yake. Anasema: “Kampeni ilidumu kwa miaka mitano, 2000 hadi 2005, na yalikuwa mafanikio makubwa, kwani wasichana na wanawake hawakeketwi tena.” Hata hivyo, anadai bado kuna watu wachache wanaoendelea kuthamini mila hiyo, hasa wahamiaji kutoka maeneo jirani, wakiwamo Wanyaturu, lakini wanakabiliwa na doria za jeshi la polisi ambalo lilikabidhiwa jukumu la kudhibiti vitendo vya ukeketaji.
(e) Katika Wilaya ya Karatu, ukeketaji unaendelea kufanyika kwa siri. Nao wanakeketa watoto wachanga. “Ukeketaji hufanywa katika maeneo ya vijijini ambapo watoto wachanga hukeketwa kwa siri pasipo kuwepo na sherehe za kimila ambazo kwa zamani ilikua ni lazima kwa zoezi kama hilo,” anasema Langew Ama wa Rhotia Kati. Anasema miongoni mwa Wairaq, mila hiyo imepungua. Anasema: “Kama ukeketaji upo ni kwa kiwango kidogo sana, tena kwa maeneo ya vijijini ambapo hufanywa kwa siri kubwa pasipo serikali kujua.”

8.0 KIPIGO KWA WANAWAKE
Vipigo kwa wanawake ni jambo lililojitokeza kila mahali. Ni tatizo kubwa la kitaifa. Katika familia nyingi, wanawake bado wanaendelea kupigwa na wanaume, hasa waume zao au wapenzi wao. Lakini wengine wanapigwa pia na viongozi wa kiserikali. Miongoni mwa sababu za wanawake kupigwa ni ulevi, “mdomo” wa akina mama, ubabe wa akinababa, fumanizi, mfumo dume, ukiukwaji wa mafunzo ya ndoa, wivu, umaskini, “mapenzi,” ndoa za mitala, ndoa za kulazimishwa nk. Sheria dhidi ya kipigo, Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 ya mwaka 2002 kifungu 240 cha kinasema kwamba mtu yeyote aliyempiga mwenzake atakuwa ametenda kosa la jinai na atahukumiwa kwenda jela kwa muda wa mwaka mmoja.
Adhabu hii itatumika katika mzingira ambayo muathirika wa kipigo hakupata madhara makubwa sana. Aidha kifungu 241 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kwa mtu yeyote aliyemdhuru mwenzake kwa kipigo na mtu huyo kupata madhara makubwa sana.

8.0.1 Visa Mikasa

(a) Katika Wilaya ya Temeke, Dar e salaam, mwaka 2011 kesi 14 ziliripotiwa. Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mbagala (PPCM) Fatuma Katunzi, anasema kesi za vipigo zipo na kwamba mwaka 2011 zilifikishwa kesi 6, kati ya kesi hizo 2 zilitolewa hukumu ya kifungo na faini. Mwenyekiti wa Mtaa wa Msufini Kata ya Chamazi, Muharami Mlawa, anasema kesi 5 ziliripotiwa katika mtaa huo. Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Majimatitu ‘B’ Kata ya Charambe Fadhil Mpinga anasema kesi 3 za vipigo zilifikishwa kwake. Ofisa Mtendaji Mtaa wa Mianzini Jimmy Berege, anasema uongozi wa mtaa huo ulipokea kesi 6 kati ya kesi hizo tatu ziko polisi.
(b) Katika Wilaya ya Simanajiro, Neema Lalashe (46) mkazi wa Kijiji cha Uhuru katika Kata ya Orukasment, anasema kuwa kwa sasa vitendo hivyo vinafanyika kistaarabu tofauti na miaka ya nyuma. Anasema: “Zamani mwanaume alikuwa anafunga mikono na miguu kwenye mti ndiyo unachapwa, unapigwa mpaka unapoteza fahamu lakini siku hizi kidogo hayo mambo yamepungua, kama umekosea atakuchapa lakini hufungwi tena na kamba.” Naye Babu Mollel (73), anasema: “Sisi zamani ulikuwa unaoa mke siyo kwa sababu unampenda, lakini ni kwa sababu huko unapooa labda hiyo familia ni maarufu na umaarufu wa huku ni kuwa na ng’ombe wengi.”
(c) Kutoka Iramba, Singida, Wandoa Edward (37) mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri, anasema: “Nataka kurudu nyumbani, kwani nimechoka kuishi katika ndoa yenye manyanyaso. Nyumba yangu si salama tena.”
(d) Wilayani Karatu, vipigo dhidi ya wanawake vipo, ingawa ni nadra kwa matukio haya kuripotiwa katika vyombo vya dola. Mtendaji wa Kata ya Karatu, Paulo Lagwen anakiri kuwepo kwa vipigo kwa wanawake kutoka kwa waume zao. “Hata hivyo, idadi ya vipigo imepungua ikilinganishwa na zaman. Wanaume wa Kiiraq wamestaarabika kidogo kwa sasa. Idadi ya vipigo imepungua ikilinganishwa na zaman. Wanaume wa Kiiraq wamestaarabika kidogo kwa sasa,” anasema.
(e) Mkoani Mbeya, zipo ndoa nyingi zilizovunjika kutokana na kipigo kwa wanawake. Watu wote 22 waliohojiwa walikiri wanaume kuwepo kwa vipigo kwa wanawake. Mkazi wa kijiji cha Mpandapanda, Lucia Gwamaka, anasema kupigwa kwa mwanamke ni jambo la kawaida. “Ndiyo tunapigwa na wanaume, lakini inakuwa vigumu kumpeleka polisi. Kwanza nawaza watoto wangu, nikimpeleka polisi nitarudi wapi?” Anahoji.
f) Wilayani Kilolo mkoani Iringa ilibainika kuwa viongozi wanapofikishwa kwenye ofisi za kijiji kwa shitaka lolote viongozi wanajichukulia sheria mkononi na kuwapiga watuhumiwa. Kwa mfano utafiti ulishuhudia kisa mkasa ambacho wanawake wawili wajawazito katika Kijiji cha Kidabaga kwa nyakati tofauti walipigwa na viongozi wa kijiji hicho na hatimaye mimba walizokuwa wamebeba zikaharibika kutokana na madhara ya vipigo hivyo.Viongozi waliohusika na vipigo hivyo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kidabaga, Nicolous Katandasi na Mtendaji wa kijiji hicho , Vincent Gaifalo .Kwa mujibu wa wanakijiji wa Kidabaga, mwenyekiti wa kijiji Nicolous Katandasi mnamo mwezi Mei 2011 alimtandika viboko vya nguvu 16 mama Silivia Kimata kitendo kilichosababisha mimba ya miezi mine ya yama huyo kuharibika. Aidha katika mwaka huu mtendaji wa kijiji hicho cha Kidabaga, Vincent Gaifalo alimchapa viboko 30 Seidina Kidwangise aliyefika kijijini hapo kumzika ndugu yake na kusababisha mimba yake kutoka na mama huyo kupata ulemavu wa kushindwa kusimama na kutembea. Mganga Mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Iringa dakta Deogratias Manyama alithibitisha kwamba hospitali hiyo mnamo tarehe 19 Aprili 2012 ilimpokea na kumlaza Seidina Kidwangise akiwa hawezi kusimama wala kutembea na uchunguzi ulikuwa umebainisha kuwa alikuwa amepoteza ujauzito na mwili wake ulikuwa na majeraha. Jambo la kushangaza wanakijiji hao walisema kuwa ingawa mtendaji wa kijiji aliyempiga mama huyo na kumsababishia madhara hayo makubwa alikuwa amefikishwa polisi, hawaamini kuwa haki itatendeka dhidi yake kutokana na kushamiri kwa rushwa hapo kijijini na kwenye vyombo vya sheria wilayani. “Ingawa wanakijiji wa Kidabaga wamechukua hatua na kuhakikisha kuwa viongozi hao wameondoka madarakani lakini hawajafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuumiza wanawake na kuharibu ujauzito wao”, alisema mwanakijiji mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuhofia maisha yake.
(g) Akina mama wa Kimasai wanapigwa lakini mila zao haziruhusu kushitaki. “Hata kama ameumizwa hawezi kusema badala yake huchinjiwa kondoo na kupewa mafuta kama tiba,” anasema Lea Saitobiki, Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji. Anasema hata kama utasikia amepigwa ukienda kumuuliza anakataa kata kata kuwa amepigwa.
Kufuatia masuala hayo kufanywa siri, hakuna takwimu zinazoonyesha tatizo la vipigo kwa wanawake lina ukubwa gani katika kata hiyo. Hata hivyo, kutokana na mahojiano na baadhi ya wananchi tatizo hilo linaonekana kuwepo kwa kiasi kikubwa, na mara nyingi linasababishwa na ugomvi wa kifamilia ambao hata hivyo, waathirika hawaripoti.
“Sisi kama serikali tunashindwa kuingilia mambo ya kifamilia, huwezi kwenda kwenye nyumba ya mtu ukaanza kuuliza wewe kwa nini unampiga mke wako wakati mke mwenyewe hajawahi kuja kuripoti,” anasema Afisa Mtendaji. Utafiti umebaini katika kata zingine zilizofanyiwa utafiti kuwa vitendo vya wanawake kupigwa hakuna takwimu kutokana na suala hilo kutoripotiwa kwenye ofisi za watendaji kata. “Haya mambo ya kupigana huwa wanayamaliza wenyewe nyumbani kwao, wakishindwa ndio wanakuja huku kwetu kushitakiana,” anasema Kaimu Afisa Mtendaji Kata ya Mwembe, Athumani Mkumbwa.

9.0 WANAWAKE NA WATOTO KUTELEKEZWA
Wanaume kutelekeza wake zao na watoto ni moja ya matukio ya kila mara katika maeneo yote ya utafiti. Utafiti huu umeonyesha kuwa sababu z kipigo kwa wanawake zinafanana na zina uhusiano na sababu zinazowafanya wanaume watelekeze wanawake. Miongoni mwa sababu hizo ni kukosa uaminifu, ugomvi usioisha, na maisha magumu. Imegundulika pia kuwa baadhi ya wanaume wanaotelekeza wake zao ni wale ambao hufanya hivyo kama njia ya kuepuka kuwapiga, kuwaumiza au kuwaua.
9.0.1 Visa Mikasa
(a) Zawadi Gwando ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Handeni, anasema malalamiko ya utelekezaji familia ni mengi eneo hilo. Anasema kwa siku nzima unaweza kupokea malalamiko yote ya utelekezaji mke na watoto katika mtizamo tofauti- wapo waliozalishwa kisha mwanaume kumtelekeza pamoja na mtoto ama mke kabisa wa ndoa kutelekezwa na watoto wake. Bi. Gwando anasema kila siku hupokea hadi kesi tatu za utelekezaji familia kutoka maeneo mbalimbali ya mji huo. “Vitendo vya utelekezaji familia vipo vingi, kwa kutwa unaweza kushinda ukipokea kesi za utelekezaji familia tu hadi mwisho wa kazi. Asilimia kubwa ya kesi za utelekezaji mke na watoto wanazopokea ni kutoka dini ya Kiislamu. Tatizo asilimia kubwa ya wakazi wa mji huu ni Waislamu ambao unakuta wana wake zaidi ya mmoja…sasa unakuta mume anatelekeza baada ya kuona hali ngumu ya maisha. Kwa upande wa Wakristu katika kesi 10 unaweza kumpata mmoja,” anasema Bi. Gwando.
(b) Wilayani Kondoa, Kaimu Mtendaji wa kata ya Suruke Jabir Issa Isere anasema athari za tatizo hili ni kubwa hasa kwa wanafunzi ambao hutelekezwa baada ya kupata mimba, hivyo pindi wanapojifungua huwaacha watoto wakilelewa kwa babu na bibi zao na wenyewe kukimbilia mijini kwa lengo la kujitafutia maisha. “Watoto na wanawake wanatelekezwa kila mara,kwani kila fedha inapopatikana katika familia nyingi badala ya kujadili ni nini kifanyike kujikomboa pale walipo wanaume huishia kutafuta mke wa pili na nyumba ndogo,” anasema. Naye Halima Mnjalo (20) Mkazi Kijiji cha Bolisa, anasema wanaume hutumia kisingizio cha kutafuta maisha na kuitelekeza familia. Anasema: “Mimi nilipata mimba nikiwa shuleni tangu mwanaume aliyenipa mimba hiyo alipofutwa aliondoka bila kuniaga wala sifahamu alipo kwani hatuna mawasiliano, hivyo jukumu la kumlea mtoto ni langu mwenyewe.”
(c) Wilayani Simanjiro, utelekezwaji unafanyika kwa wanaume kuondoka majumbani kwao na kuwaacha wanawake wakiendesha familia mbazo ni kubwa ama kuendelea kuishi nao lakini shughuli zote za familia wakiachiwa wao. Ana Moreta (49) mkazi wa Kijiji cha Narokusoito kata ya Langai ana mzigo wa kuendesha familia yenye watoto wanane baada ya mume wake kuondoka nyumbani na kwenda kusikojulikana. Kutokana na kutokuwa na mashamba wala mifugo, kwa sasa mama huyo analazimika kuendesha familia yake kwa biashara ya kuuza ugoro na maziwa kidogo anayoyauza baada ya kukamua ngombe wake wawili. Anasema kuwa, mume wake alitoweka nyumbani miaka tisa iliyopita na kwenda kusikojulikana.
“Mimi na mke mwenzangu tuko kwenye boma la mume wetu lakini hatujui alipo, yeye aliondoka tu hatujui alienda wapi,” anasema. Mama huyu anasema kuwa, baada ya kuona maisha yanazidi kuwa magumu, aliamua kwenda nyumbani kwao kuomba ng’ombe wawili anaowakamua kwa sasa.
(d) Kutoka Kilolo, Iringa, Ofisa Ustawi wa Jamii wa wilaya, Piencia Mushi, anasema: “Kuhama kwa wanaume kwenda mijini, nchi za jirani ikiwemo Msumbiji, kwenye mashamba makubwa ya mbao kufanya vibarua imekuwa ni moja ya sababu ya kutelekeza wanawake na watoto.”
(e) Kutoka Mvomero, Mkazi wa Kijiji cha Kidudwe, Kata ya Mtibwa, ambaye ni mwathirika wa kutelekezwa, Ester God, anasema katika miaka 10 alioishi na mumewe, ametelekezwa mara tatu. Mara ya mwiho jambo hilo lilimtokea akiwa na mtoto wa mwezi mmoja. “Baada ya kunitoroka na kuniacha na kichanga cha mwezi mmoja, nilijizoazoa na kuanza kuuza mboga ili kuwezesha watoto wangu wengine waendelee na shule na kupata chakula,” anasema.
(f) Wilayani Tarime, Mara, mkazi wa kijiji cha Korotambe, Christina Kyangwi, anasema mila ya Kikurya humruhusu mwanamume kuoa wanawake zaidi ya watatu. “Sasa kama kipato cha mwanamume ni kidogo, hulazimika kuikimbia familia yake moja na kuhamia kwenye familia yake nyingine, na tabia huendelea nayo na hatimaye kuondoka kabisa kijijini hapo.” Anasema kwamba kitendo cha kutelekezwa na mume wake na kuachwa na watoto wake wawili, kimemuathiri sana kisaikolojia na kumsababishia kupata maradhi ya moyo ambayo sasa yanamsumbua mara kwa mara. Kutokana na hali yake ya maisha kuwa duni, anashindwa kuwalea vizuri watoto wake kwani malezi mazuri hutokana na baba na mama wawapo pamoja. Akielezea athari nyingine, alisema ni rahisi sana kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwani itamsababishia kutafuta mwanamume mwingine wa kumpatia riziki ili kujikimu kimaisha.
10.0 HITIMISHO
Utafiti huu umedhihirisha kuwa unyanyasaji wa kijinsia ni ya maisha ya Watanzania. Wanawake na wasichana wengi wanafanyiwa vitendo vya kikatili na hawatoi taarifa popote kwa hofu ya kupata aibu au kutengwa na jamii. Baadhi ya sheria zilizopo hazikidhi matakwa, na nyingine zinakinzana. Vile vile, uelewa wa jamii kuhusu haki zao na wajibu wao na serikali ni mdogo. Umaskini unaendelea kuwa kisingizio cha unyanyasaji, hasa vijijini. Kwa sababu hiyo, watunga sheria na viongozi husika katika jami wanawajibika kuongoza harakati za kuondoa mazingira haya mabaya yanayodunisha maisha ya wananchi, hasa wanawake na watoto. Serikali inapaswa kuboresha mazingira vijijini, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu mbadala ili kuondoa kero zinazosababisha uduni wa maisha unaotumiwa kuendeleza unyanyasaji wa kijinsia.
Lakini zaidi taasisi za umma na za kijamii zinapaswa kubuni mipango itakayoweza kuhamasisha umma kuacha kunyanyapaa waliofanyiwa ukatili kama vile kubakwa. Aidha wanapashwa kuchukua hatua kuhakikisha wanaotuhumiwa kwa makosa ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji wananchi wanachukua jukumu la kumsaidia kupata na kutunza ushahidi na hatua za kisheria kuchukua mkondo wake.
Matokeo ya utafiti huu yatasaidia katika kuwafanya viongozi wa siasa na watendaji wa Serikali kupima kile walichofanya kama kimesaidia kumaliza matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yao. Taarifa kwamba viongozi hao hufumbia macho suala la ukeketaji, zitasaidia kuvipa vyombo vingine njia za kuwafuatilia na kuwawajibisha viongozi wazembe. Pia taarifa za kukuketwa kwa watoto wadogo, zinatoa fursa kwa wadau wa sekta ya afya na jinsia kufanya uchunguzi juu ya hali hii na kubuni njia mbadala za kuzuia unyanyasaji huu.
Ni dhahiri kwamba athari za unyanyasaji huu ni nyingi na za hatari, hasa kwa kizazi kijacho. Hivyo, ni vema serikali ichukulie kwa uzito wa pekee taarifa ili kuandaa mikakati ya kunusuru taifa kutoka kwenye unyanyasaji huu ambao unaweza kukatisha maisha ya baadhi ya wanajamii, na kudunisha maendeleo ya jamii huko tuendako.
Wazazi na viongozi wa jamii, hasa wa dini, wana jukumu la kuongeza nguvu katika kutoa malezi bora na mafundisho mwanana ya kiimani, kama njia ya kutokomeza tabia zitokanazo na mazoea mabaya na ukosefu wa uadilifu.