KUTOKANA na hali ya huduma ya miundombinu ya usafirishaji kuwa duni na ya aghali imeshindwa kukuza biashara na uchumi katika kiwango kinachotegemewa katika mataifa mengi ya barani Afrika. Sekta ya huduma ya miundombinu ambayo ni kichocheo kikubwa katika kukua kwa uchumi imeshindwa kuleta mageuzi ya kutosha.
Taarifa hiyo imebainishwa katika Ripoti ya UNCTAD ya Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika ya Mwaka 2015 iliyozinduliwa Jijini Geneva na kusoma katika baadhi ya mataifa ya Afrika. Akifafanua ripoti hiyo nchini Tanzania, Ofisa Mwandamizi anayeshughulikia Masuala ya Uchumi UN, Laura Paez alisema huduma za miundombinu ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya 2016-2030 na kujenga jukwaa kwa ajili ya ukuaji mpana barani Afrika.
Alisema katika ripoti hiyo inayotoa mwangaza wa uchumi wa Afrika imebainisha huduma za miundombinu kama vile maji na afya zinahusishwa zinahusishwa na malengo muhimu ya maendeleo endelevu katika kufikia matokeo ya maendeleo ya kijamii na endelevu. Alisema huduma kama vile umeme, mawasiliano ya simu na usafiri huchangia katika tija pia huamuwa ushindani wa makampuni ya Afrika.
“Afrika inawakilisha asilimia 15 ya idadi ya watu duniani lakini inatoa asilimia 2.2 tu ya huduma za mauzo ya nje kimataifa, hali hii inaonesha kutotumika kikamilifu kwa sekta hiyo,” anafafanua Katibu Mkuu wa UNCTAD Mukhisa Kituyi akizungumzia ripoti hiyo ya Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika ya Mwaka 2015.
Aliongeza kuwa ripoti ya Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika ya Mwaka 2015 inasisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika kukabiliana na changamoto za mapungufu mbalimbali katika udhibiti wa sera, ambayo yamechangia kukosekana kwa ufanisi wa kuweza kutumia kikamilifu sekta ya huduma kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Ripoti hiyo pia inabainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2009-2012 sekta ya huduma barani Afrika ilikuwa kwa kiwango cha asilimia 4.6 ikilinganishwa na asilimia 5.4 katika nchi zinazoendelea. Sekta ndogo za kihuduma zilizokuwa kwa kasi zaidi zilikuwa usafiri, uhifadhi na mawasiliano.
Hata hivyo sekta ya huduma katika Afrika iliongoza ukuwaji wa pato la taifa katika chi 30 kati ya nchi 54 katika kipindi cha 2009-2012, huku kati ya nchi 45 ambapo pato la sehemu ya huduma lilipanda, 30 zilipata tatizo la kupungua kwa uzalishaji viwandani kuanzia kipindi cha 2001-2004 hadi kipindi cha 2009-2012.
Aidha alisema baadhi ya nchi za Afrika zimeendeleza huduma za viwanda vyao kwa mafanikio na hata zinapeleka huduma zake katika masoko ya Afrika huku akizitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Mauritius na Nigeria ambapo zinafanya vizuri sekta ya huduma za kifedha na kibenki. Alisema kibiashara katika sekta ya usafiri wa anga nchi za Ethiopia, Kenya na Afrika ya Kusini zinafanya vizuri huku huduma za elimu ni Uganda, huduma za mawasiliano ya simu Misri na huduma za Bandari ni nchi ya Djibouti na Kenya.
Baada ya ufafanuzi huo ripoti imeshauri masuala kadhaa ikiwemo kuwa na kanuni ya ufanisi wa huduma ya miundombinu. Alisema pamoja na hayo mataifa mengi yapo chini katika uhuru udhibiti sekta zote na mifano ya viwango vya kimataifa vya udhibiti wa miundombinu havitumiki barani Afrika ilhali vyombo vingi vya udhibiti vipo katika hatua za awali za maendeleo na bajeti ya kawaida na mara nyingi hata hukosa wafanyakazi wenye sifa.