Mtoto wa Rais, Dk. Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete amemshukia aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Arusha, James Ole Millya.
Millya alijiengua kutoka CCM na kujiunga CDM kutokana na kile alichoeleza kuwa chama tawala kimekuwa mfano wa gari lililosheni pancha, hivyo halifai kwa safari.
Hata hivyo, baada ya Millya kuondoka CCM, taarifa zilizopatikana mkoani humo zilieleza kwamba aliondoka akiwa na takribani Shilingi milioni 2, mali ya UVCCM.
Taarifa hizo ndizo zimemuibua Ridhiwani akichangia katika mtandao wa kijamii wa Tunuru la Afrika na kusema Millya asubiri utaratibu unafuata.
Ridhiwani aliandika maneno hayo juzi kupitia simu yake ya mkononi na kuyatuma kwenye mtandao huo akisema, “nilidhani utani, kumbe James (Millya) tunamdai hela za Umoja wa Vijana mkoa wa Arusha.”
Aliongeza, “nawashukuru vijana makini wa mkoa wa Arusha kwa umakini wa hali ya juu. Utaratibu waja bwana Millya kama unasoma post hii.
Hata hivyo ujumbe huo wa Ridhiwani ulichangiwa na washiriki mbalimbali, wengi wao wakimpinga na kumhusisha (Ridhiwani) na familia yake kwa tuhuma zenye nia ovu.
Baadhi ya tuhuma hizo zimewahi kuchapishwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari, zikikariri vyanzo tofauti.
Millya alitangaza kujiudhuru uwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha hivi karibuni na kuhamia rasmi katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Aidha, siku iliyofuata viongozi wa CCM kwa nyakati tofauti walikaririwa na vyombo vya habari wakimwelezea Millya kuwa, alikuwa gamba na mzigo ndani ya chama umoja huo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI