Na Ngusekela David, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Chiku Ngalawa amefanya ziara fupi katika vitalu vya miche ya machungwa vinavyozalishwa na wakulima wa Kikundi cha Maduma kilichopo Kijiji cha Maduma Kata ya Mtindiro wilayani Muheza.
Kiongozi huyo akiwa eneo la tukio amesifu juhudi zinazofanywa na wakulima wa Maduma na kuwashauri kuwa karibu na wataalamu wa kilimo ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri fursa zilizopo hususan Mradi wa Muungano wa Wajasiriamali Vijijini (MUVI), kuhakikisha wanazalisha kwa wingi aina mpya ya miche isiyo na mbegu yaani ‘seedless’ kwani ndio njia pekee ya kulishika soko la ndani na nje ya nchi.
Kikundi hicho chenye wanachama 12 kina jumla ya ekari atu ambazo zina miche isiopungua 50,000, mbali na miti ya machungwa 30 ambayo tayari inamachungwa. Mradi wa MUVI tangu kuanzishwa kwake umekua ukishirikiana kwa karibu na kikundi hicho ili kuhakikisha wanaunganishwa na huduma wanazozihitaji kwa haraka na uhakika.
Awali Mradi wa MUVI ulitoa miche ipatayo 5,000 aina mpya ya valecia ambayo haina mbegu ndani (seedless) ambapo mpaka sasa miche hiyo imekwisha kuungiwa (budding) katika miti ya malimao huku mingine ikiuzwa kwa watu mbalimbali mkoani hapa. Vile vile Mradi umewaunganisha wana kikundi hawa na Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) na kupatiwa mkopo wa fedha taslimu milioni 2, ambazo zimetumika kununua pampu ndogo ya kusukuma maji ya kumwagilia miche kipindi cha kiangazi.
Wakielezea mafanikio yao wanachama hao wameushukuru mradi wa MUVI kwa kuwa ni sehemu kubwa ya mafanikio yao kwani hapo awali walikua na tatizo la namna ya kumwagilia miche hiyo lakini kupatikana kwa pampu hiyo imekua ni chachu kubwa katika ukuaji wa miche hiyo. Mradi wa MUVI unafadhiliwa na shirika la kimataifa la maendeleo ya kilimo chini ya Wizara ya Viwanda Biashara na Masoko na kusimamiwa na SIDO.