Na Atley Kuni, Ofisa Habari Mwanza
SERIKALI mkoani Mwanza imesema hakuna kulala hadi mtoto Pendo Emmanuel (Albino) apatikane kufuatia tukio la kutekwa na watu wasiojulikana toka tarehe 27.12.2014 katika kijiji cha Ndami, Tarafa ya Mwamashimba Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza na kisha kutoweka naye kwenda kusiko julikana hadi sasa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo na kuwahusisha wananchi wakijiji hicho pamoja na uongozi wa Wilaya na Mkoa huku akitaka kujua hatua iliyofikiwa na wana nchi hao katika kuwabaini walifanya unyama huo.
Mtoto Pendo alitekwa na watu wasiojulikana mnamo usiku wa tarehe 27.12.2014 majira ya saa nne usiku akiwa amelala na wazazi wake huko Nyumbani kwao na kisha watekaji kutoweka naye na kwenda kusiko julikana hadi sasa, huku taarifa za Polisi zikionesha jumla ya watu kumi na watano (15), wakiendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Akihutubia wananchi wa kijiji hicho Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisema ni tukio la kusikitisha kwani toka mwaka 2007 hakuna tukio la namna hiyo lililo wahi kutokea katika Wilaya hiyo na tukio la mwisho lililotokea lilimkumba mwananchi wa Wilaya hiyo aliyekuwa amesafiri kwenda Mkoani Shinyanga kwa shughuli zake.
Amesema kiburi walicho nacho watekaji hakiwezi kuwa nje ya mipaka ya kijiji hicho cha Ndami bali mpango mzima unajulikana kwa wenyeji na ndio maana ilikuwa rahisi kufanya unyama huo “Kiburi cha watekaji kimo humu humu haiwezekani mtu kutoka mbali aje atekeleze tukio hapa kijijini bila yakuwa na wenyeji lazima kuna mtu au watu walioshirikiana na wahalifu hao”, alisema Mulongo na kuongeza “ kwa mazingira ya Nyumba ya kina Pendo ilipo kule hakuna sehemu yakutokea na kama mliona pikipiki inaranda randa mchana,..iweje mshindwe kuitilia shaka? Hapana, hii haikubaliki! mimi nimekuja kuwaambia nataka Pendo apatikane na sio vinginevyo, nawapa siku tano ijumaa nitarudi hapa mniambie Pendo yuko wapi! Alisema mkuu huyo wa Mkoa akionesha kusononeshwa na tukio hilo.
“Mbona mifugo inapo ibwa inapatikana”? Aliwahoji viongozi wa sungu sungu na kusema haiingii akilini kusema wakati wa tukio la utekaji sungu sungu wote walikuwa wamekwenda kula chakula na ndipo kadhia hiyo ilipotokea, mkuu wa mkoa, alihoji kufatia kauli iliyotolewa na kiongozi wa sungu sungu kuwa wakati wa tukio askari wote wa sungu sungu walikuwa wamekwenda kula majira ya saa tatu na tukio kutokea saa nne.
Awali akielezea kusikitishwa kwake na tukio hilo, Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa Ngozi mkoani hapa Alfred Kapole, alisema inasikitisha kuona wanadamu wakiwauwa binadamu wenzao kama vile wanyama bila hata woga na vyombo vya maamuzi vikishindwa kutoa hukumu kwa wakati huku akielekeza lawama zake kwa mahakama na Mkemia Mkuu. “Mh. Mkuu wa mkoa inasikitisha kuona miongoni mwa kesi 72 zilizokuwa mahakamani, ni kesi 3 tu ndizo zilizokwisha kutolewa hukumu” alisema Kapole, na kuongeza ingekuwa ni kesi ya Wabunge wameshindana kwenye masuala ya uchaguzi ingekuwa imekwisha hukumiwa lakini kwakuwa ni mlemavu wa ngozi, basi kupuuzia kumekuwa kwingi mno. Alisema kapole.
Akinukuu maneno kutoka katika kitabu cha Biblia, Kapole alisema hata kama hukumu zitashindwa kutolewa na wanadamu hapa Duniani, naamini Mungu wa Mbinguni kuna siku haki itatendeka kwa kuwa “Kitabu cha Mika 3.3-7 kinaeleza juu ya hukumu watakayo ipata watu walao nyama za watu bila woga. Kesi zinaendeshwa Polisi wanajitaihidi sana lakini mkemia watendaji wa ofisi ya mkemia mkuu wanatuhujumu kwa kuita nywele zetu albino ni za Midoli, aling’aka Kapole wakati akielezea kusikitishwa na ofisi ya Mkemia mkuu wa serikali pindi inapo pelekewa Nywele.
Mwenyekiti Kapole pia aliomba kwa yeyote aliye na Mtoto huyo kumrejesha na kama wamemdhuru basi warejeshe hata mwili wake ili matanga yaweze kufanyika, akatumia fursa hiyo kumomba Rais wale wote waliohukumiwa kunyongwa wanyongwe ili kuepusha kuendelea kula chakula cha serikali bure.
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa aliwataka wanachi kuweka mbali itikadi zao za namna yoyote na kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha zoezi zima la kuwasaka walio husika na utekaji wa mtoto Pendo Emmanuel, ambao unasimuliwa kuleta siamanzi kubwa ndani ya jamii ya wana Kwimba na watanzania lakini pia kuchafua taswira ya nchi mbele ya mataifa mengine ya Dunia. Huku akiwaonya watu wa haki za binadamu kuacha kupaza sauti za kuwatetea wahalifu. Tanzania inatajwa kuwa kinara cha ukatili huo tangu mauwaji hayo yalipo zuka mwanzoni mwa miaka ya 2006/2007.
Kwa Mujibu wa takwimu za kimataifa zinaonesha ni asilimia 2% tu ya watu ambao huzaliwa na ulemavu wa ngozi ndio hufikia na kusherekea miaka 40 ya kuzaliwa kwao, huku pia takwimu zikionesha katika nchi za Afrika mtu mmoja (1) kati ya elfu mbili (2000) huzaliwa wakiwa na ulemavu wa ngozi wakati katika marekani ni mtu mmoja kati ya elfu kumi na saba ndio huishi na ulemavu wa ngozi.
Mauaji ya Albino katika Tanzania yanaonekana kushamiri katika Mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo imani za kishirikina zikitajwa kuwa chanzo kikubwa cha mauwaji ya hayo lakini pia yale yalio wahusu vikongwe yanayo husishwa na masuala ya kujipatia utajiri wa haraka suala ambalo sio la kweli, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mauwaji yalianza siku nyingi japo kuripotiwa katika mamlaka za serikali na vyombo vya habari ilianza mwaka 2006/2007.
Hivi sasa zipo asasi za kiraia zinazo jihusisha na harakati za kupinga mauwaji hayo ikiwapo asasi ya Under The Same Sun ya Nchini Canada na kwa Tanzania imeshakuwa na tawi toka mwaka 2008. Awali akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mulowola alisema tayari watu 15 wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani humo kwa mahojiano zaidi akiwapo baba mzazi wa Pendo, lakini pia jeshi hilo limefanikiwa kuipata piki piki iliyotumika kufanya unyama huo.
“Hivi sasa tunawashikilia watu wapatao kumi na watano na wanaendelea kuhojiwa na Polisi” alisema Mlowola na kuongeza kuwa huo sio mwisho kwa kuwa jinai haina mwisho hata miaka ishirini tukio hili litaendelea kuchunguzwa”, na kusema hata kama yeye atahamishwa au kustaafu kijana atakayekuja ataendelea na kesi hiyo, hivyo wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa kile wanacho kifahamu, alisema Mlowola na kusema tayari Jeshi hilo mkoani hapa limetangaza kuto Milioni tatu 3 kwa atakayefanikisha kupatikana kwa mtoto Pendo. Mtoto Pendo alikuwa ni miongoni mwa alibino 74 waliopo katika wilaya ya Kwimba na alikuwa namba 9 katika suala la kupatiwa ulizi.