MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na Msanii maarufu wa kughani mashairi katika nyimbo, Mrisho Mpoto wameahidi kuisaidia magodoro 110 Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kiislamu ya Ilala iliyoteketea kwa moto juzi usiku.
Mkuu wa Mkoa Makonda ameahidi kutoa magodoro 100 alipoitembelea shule hiyo inayomilikiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kiislamu (IDF), kwa ajili ya kutoa pole na kuangalia madhara yaliyotokea katika ajali hiyo. Katika ziara hiyo msanii Mpoto naye aliahidi kutoa magodoro 10 ikiwa ni kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa kwa ajali hiyo ya moto.
Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa aliambatana na maofisa mbalimbali kutoka mkoani ikiwa ni kujionea uharibifu uliosababishwa na moto huo na kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi ili waweze kuendelea na shule kama ilivyo kuwa hapo awali. RC Makonda aliwataka wananchi na taasisi mbalimbali zijitokeze kusaidia ajali hiyo muda huu ambapo uchunguzi wa ajali ukiendelea ili wanafunzi wapate mahitaji muhimu na kuendelea na masomo yao.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum naye akiwa na viongozi anuai wa dini ya Kiislamu walitembelea na kupata maelezo ya ajali hiyo mapema leo jijini Dar es Salaam. Moto huo mkubwa uliyoiteketeza shule hiyo pamoja na vifaa mbalimbali vya wanafunzi uliibuka jana majira ya saa tatu kasoro usiku. Hata hivyo haijulikani chanzo cha moto huo kwani muda ambapo uliibuka hakukuwa na umeme
katika majengo yaliyoungua. Bado jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo.