MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amehojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa saa tatu kuhusiana na tuhuma zinazomkabili. Makonda anatuhumiwa kuingilia haki, uhuru na madaraka ya Bunge.
Taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Bunge jana, zilisema Makonda aliwasili bungeni Dodoma jana saa nne asubuhi kuitikia wito wa kamati hiyo uliotokana na azimio la Bunge lililotolewa Februari 8 mwaka huu, katika Kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita wa Bunge. Katika kikao hicho, Bunge liliazimia Makonda pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arumeru, Alexander Mnyeti, kuitwa mbele ya kamati hiyo kujibu tuhuma zinazowakabili.
Akizungumza mara baada ya kamati hiyo kumaliza kazi yake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Mkuchika, alisema walimuhoji Makonda baada ya kuagizwa na Spika.
“Kamati imekutana baada ya kuagizwa na Spika kwa mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge. Aliagiza tumuite Makonda kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema Mkuchika.
Alisema kwa mujibu wa Azimio hilo, Makonda anadaiwa kutoa kauli kupitia kituo cha luninga cha Clouds akidai kwamba wabunge wanaokosoa hatua yake ya kutaja hadharani majina ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya huenda wananufaika na biashara hiyo. Mkuchika alisema kamati imemaliza kumuhoji na itakabidhi taarifa kwa Spika ambapo ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa.
Makonda aliingia kwenye mzozo na Bunge siku chache baada ya kutaja orodha ya watu 12 na wasanii mbalimbali akiwamo Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kabla ya kutaja orodha nyingine ya wanasiasa, viongozi wa dini pamoja na wafanyabiashara. Katika orodha ya pili ya watu 65, Makonda aliwataja Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephati Gwajima pamoja na mfanyabiashara maarufu nchini, Yusufu Manji.
Kutokana na hatua hiyo wabunge walikuja juu na kuonyesha waziwazi kukerwa na hatua aina hiyo ya Makonda wakidai haina nia njema katika vita hiyo ya dawa za kulevya. Kutokana na mijadala iliyokuwa ikiendelea bungeni, Makonda alinukuliwa akisema kuwa hawezi kujishughulisha na kauli za wabunge kwani kazi yao ni kulala na wengine wako kwa ajili ya kuchekesha wenzao.
Kauli hiyo iliibua mjadala mkali bungeni ambapo Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), aliomba mwongozo kwa Naibu Spika akidai kuwa Makonda amelidharau Bunge. Alisema kauli hiyo haiwezi kukubaliwa kwa sababu nao wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya dawa za kulevya kama anavyofanya mkuu huyo wa mkoa.
“Makonda amezungumza na vyombo vya habari na ametoa lugha za dharau kwa Bunge kwamba kazi yetu sisi wabunge ni kulala. “Sisi wabunge tuko mstari wa mbele kupambana na kumsaidia Rais Dk. Magufuli katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
“Ikumbukwe kwamba, hiyo sheria ya dawa za kulevya imetungwa na Bunge hili na kama haitoshi, siku rais alipokuja kuzindua Bunge hili tulimpigia makofi aliposema atapambana na dawa za kulevya. “Makonda ni mdogo wangu, ni kijana mwenzangu na ni rafiki yangu, lakini Bunge lazima liendelee kuheshimika kwa namna yoyote ile,” alisema Ulega.
Baada ya majadiliano wabunge walipendekeza mkuu huyo wa mkoa awaombe msamaha wabunge kwa kulidhalilisha Bunge, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, atoe tamko na Bunge liandike barua kwa Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo wabunge kwa pamoja walikataa hoja ya Waziri Mkuu kuzungumza kwa niaba ya serikali na badala yake walikubaliana Bunge liandike barua kwenda Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumtaka Makonda kuliomba Bunge radhi.
Baada ya uamuzi huo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alikaririwa akisema kwamba uamuzi huo haukufuata utaratibu. Hatua hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya wabunge na kuomba mwongozo kuhoji kwa nini katibu huyo ametoa kauli ambayo inakinzana na makubaliano ya Bunge. Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alitaka Bunge lijadili na kutoa maazimio ili kurejesha heshima ya chombo hicho, hoja ambayo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliipokea na kutoa nafasi kwa wabunge kujadili na baadaye kuipitisha kwa kauli moja.
Bunge lilipitisha maazimio manne likiwamo la kuitwa kwa wateule hao wa Rais baada ya matamko yao kwa nyakati tofauti ambayo yalionekana kudharau na kuingilia madaraka ya chombo hicho. Azimio lingine ni kumtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutoingilia majukumu yasiyowahusu.
CHANZO: mtanzania.co.tz/saa-3-tatu-ngumu-kwa-makonda/