Na EmanuelMadafa,Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla ameagiza kukamatwa kwa mmiliki wa kampuni ya Kundan Singh, ambaye alipewa tenda ya kujenga uwanja wa ndege wa Songwe, baada ya kushindwa kulipa mafao ya vibarua zaidi ya 50.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya ametoa kauli hiyo , wakati akijibu na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa kipindi kirefu, hali iliyochangia wananchi kuichukia serikali kwa madai ya kushindwa kuwatendea haki.
Awali, akitoa malalamiko hayo kwa Mkuu wa Mkoa, Joshua Mwasilonde kwa niaba ya vibarua wenzake, amesema wamekuwa wakidai mafao yao tangu mwaka 2012/2013 katika mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF na kwamba kila wanapofuatilia wamekuwa wakipigwa kalenda.
Akilizungumzia hilo, Makala amesema, kwakua serikali iliingia mkataba na kampuni hiyo na kumalizana nayo bila ya kuacha deni lolote hivyo mkandarasi huyo anapaswa kuwalipa vibarua hao na kuutaka uongozi wa NSSF, kuhakikisha unavishirikisha vyombo vya dola katika kumkamata mkandarasi huyo.