RC Kilimanjaro aziasa kamati za sensa Wilaya

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama

Na Mwandishi Wetu, Moshi

SERIKALI mkoani Kilimanjaro, imeziagiza kamati zinazoratibu zoezi la
sensa ya watu na makazi wilaya, kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili kuweza kuwapata makarani makini, watakaotekeleza jukumu hilo kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi ya taifa. Mbali na hilo mkoa huo pia umevitaka vyombo vya dola kuhakikisha wakati wote wa zoezi la sensa hali ya amani na utulivu inaimarika na pasiwepo na mtu au kikundi chochote ambacho kitavuruga zoezi hilo.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama,
wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusu
mchakato wa maandalizi ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa
kufanyika nchini kote kuanzia Agosti 26, mwaka huu.

Gama alisema walioomba nafasi ya ukarani wa Sensa kwa mwaka huu ni
wengi sana hivyo ili kuweza kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kama
ilivyokusudiwa na serikali kamati za uratibu katika ngazi za wilaya
hazina budi kuwa makini katika uteuzi huo.

Alisema kazi ya sensa ni kubwa na ngumu kuliko fedha watakazolipwa
makarani hao, hivyo kamati hizo zihakikishe zinateua watu ambao ni
makini,tulivu na wazalendo na nchi yao ambao watasimama kuhakikisha
zoezi hilo linafanikiwa.

“Zoezi hili la sensa ni ngumu sana, hivyo nazitaka kamati za wilaya
kuwa makini katika uteuzi wa makarani na zihakikishe zinateua watu
ambao ni makini na wazalendo ambao wataweka maslahi ya taifa
mbele,” alisema Gama.

Aidha Gama alisisitiza kuwa zoezi la sensa halitaathiri shughuli
zozote za kiuchumi, hivyo ni vema wananchi wote wakahakikisha
wanashiriki zoezi hilo kwa ukamilifu ili kuwezesha kupatikana kwa
takwimu sahihi.

Katika hatua nyingine Gama aliwataka wakuu wa kaya kuhakikisha
wanatunza kumbukumbu za taarifa mbalimbali za watu waliolala katika
kaya zao usiku wa kuamkia Agust 26 ili kuwezesha kupatikana kwa
taarifa sahihi pindi watakapofika makarani wa sensa.

Alisema taarifa ambazo zitahitajika ni pamoja na Jina kamili, Umri, Kiwango cha elimu, Jinsia, Shughuli za Kiuchumi, Mahali anapoishi, Anaposhinda, Hali ya Ndoa kama ameoa au olewa na watoto aliowahi kuwazaa. Hata hivyo Gama aliwaondoa wasiwasi wananchi mkoani humo kuwa taarifa watakazozitoa zitakuwa ni siri na kwamba zitatumika tu kwenye masuala ya kitakwimu na si vinginevyo.

Mkuu huyo alitoa pia wito kwa viongozi wa kisiasa, dini na serikali katika
ngazi zote kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye zoezi hilo la sensa hatua ambayo itawezesha kufanikiwa kwa zoezi hilo ambalo ni muhimu katika nchi. Mkoa wa Kilimanjaro una jumla ya vituo vilivyoainishwa 3,357. Vikiwa vya dodiso fupi 2,337 na vituo vya dodoso refu 1,020 ambapo makarani ni 6,714 na wasimamizi ni 350.