Na Mwandishi Wetu, Moshi
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amemuamuru Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Singa wilayani Moshi, Onesmo Chuwa kuwachukulia hatua watu waliowasha moto eneo la maporomoko kitongoji cha Singa juu kwa madai ya kuandaa mashamba kinyume cha sheria.
Gama ametoa siku tatu kwa mtendaji huyo kuhakikisha amewatia katika mikono ya sheria watu hao ambao wameonekana kukiuka sheria ya mazingira inayokataza kuendesha shughuli za kilimo kando kando ya vyanzo vya maji na kwenye kingo za mito.
Gama alitoa agizo hilo mara baada ya kupita eneo la kitongoji cha singa juu na kukuta kumewashwa moto huku mtendaji huyo akiwa hajui nini ambacho kinaendelea katika maeneo hayo ambayo ni ya maporomoko na hakuruhusiwi kuendeshwa shughuli za kilimo wala kukatwa miti.
Kufuatia tukio hilo mkuu huyo wa mkoa amemuagiza mkuu wa wilaya ya Moshi Ibrahimu Msengi, kumuweka ndani mtendaji wa kijiji cha Singa endapo hata wakamata watuhumiwa wa uharibifu wa mazingira katika kijiji hicho kitongoji cha singa juu ndani ya siku tatu ambazo amempa.
“Mtendaji nakupa siku tatu watu waliowasha moto katika eneo la maporomoko wawekwe ndani, Dc kama mtendaji huyu hatawaweka watu hawa ndani mweke ndani yeye kwani tumeshakubaliana kwamba, tusikate miti, tusilime kando ya mito, kwenye kingo za mito wala kwenye vyanzo vya maji na tusimamie kauli ya Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete, Tumekata miti kama mwenda wazimu na sasa tupande miti kama mwenda wazimu,” alisema Gama.
Mkuu huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuacha kulima maeneo ya kingo za mito na badala yake kufuga nyuki katika maeneo hayo ikiwa ni njia moja wapo ya kuhifadhi mazingira na kujiongezea kipato.
Alisema kuna haja ya wananchi wote kuunga mkono jitihada za serikali ya mkoa huo za kudhibiti uharibifu wa mazingira ili kuweza kurudisha hali ya mazingira ya mkoa huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na kuwezesha kupatikana kwa maji kwaurahisi kama zamani.
Alisema ni vema pia viongozi wa vijiji na kata wakasimama vema katika nafasi zao na kuhakikisha wananchi wanafuata sheria za mazingira na kwa atakayebainika kukiuka sheria hizo, awajibishwe ili kukomesha tatizo la uharibifu wa mazingira.