Na Kibada Ernest Kibada, Katavi
MKUU wa Mkoa wa Katavi Dk. Ibrahimu Msengi ameagiza wanafunzi wote waliohitimu Elimu ya Msingi mwaka 2014 na kuchaguliwa kujiunga na Elimu ya Sekondari waripoti katika shule walizopangiwa kuhudhuria masomo yao.
Alitoa kauli hiyo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Mstaafu Issa Seleman Njiku wakati akifungua kikao kazi cha Viongozi, Wataalamu wa Elimu Mkoani Katavi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Shule ya Sekondari iliyonga wilayani Mlele.
Mkuu huyo wa Mkoa amehimiza kukomeshwa kwa watoro mashuleni wanafunzi walioacha shule wasakwe na kurudishwa shuleni ili waendelee na masomo, akasema watoro hao ni wale ambao wenzao wanaendelea shule kwa sasa.
Amewaagiza Viongozi hao kuhakikisha uandikishaji wa wanafunzi Elimu ya Awali unafanyika na kila Shule ya Msingi kuwe na Darasa la kwanza Elimu ya Awali, miaka inavyosonga mbele uandikishaji unashuka sana na hasa kwa elimu ya Awali.
Akizungumzia ukamilishaji wa ujenzi wa maabara kila Shule ya Sekondari iwe na maabara inayofanya kazi na ifikapo machi 30 mwaka huu Halmashauri zinatakiwa zimkabidhi Maabara hizo zikiwa zimekamilika kila kitu, kuanzia majengo, vifaa na miiundombinu yote muhimu inayohitajika na iwe inafanya kazi.
Awali Ofisa Elimu Mkoa wa Katavi Ernest Hinju katika taarifa yake ya Mkoa kuhusu maendeleo ya taaluma alisema kuwa Mkoa umepiga hatua kubwa kimaendeleo kwenye sekta ya Elimu kitaaluma, katika matokeo ya kuhitimu elimu ya Msingi, matokeo ya darasa la saba mwaka 2014 Mkoa umefanya vizuri.
Hinju alieleza kuwa matokeo yanaonesha Halmashauri ya Mji wa Mpanda ilishika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na ufaulu wa asilimia 90, hivyo kuufanya Mkoa ulishika nafasi ya 11 kitaifa ulipanda kwa nafasi tatu 3 kitaifa. Takwimu zinaonesha kuwa matokeo ya darasa nne kwa mwaka 2014 ambapo Mkoa umefaulisha wanafunzi 8514 kati yao wanafunzi 9931 sawa na asilimia 85.73 hali ambayo ni mafanikio makubwa.
Kwa upande wa matokeo ya darasa saba 2013 Mkoa ulifaulisha wanafunzi 3769 kati ya 8142 sawa na asilimia 46 ya na hivyo kushika nafasi ya 13 kati ya Mikoa 25. kwa Mwaka 2014 matokeo ya darasa la saba mkoa umefaulisha wanafunzi 4419 kati ya 7240 sawa na asilimia 61.04 na hivyo mkoa kushika nafasi ya 11kati ya mikoa 25, Mkoa umeshika nafasi ya 3 kitaifa na Halmashauri ya Mji wa Mpanda.
Akizungumzia mtihani wa kidato nne mkoa umepata ufaulu wa asilimia 69 na kufikia malengo na shule ya sekondari usevya ilishika nafasi 38 kati ya shule 268 za kitaifa katika matokeo ya mtihani kidato cha sita. Pamoja na mafanikio hayo pia zipo zipo changamoto kadha ambazo zinaikabili sekta ya Elimu Mkoa baadhi ya changamoto hizo ni uhaba wa madawati, upungufu wa madarasa na nyumba za walimu, maabara, baadhi ya shule kutoa chakula mashuleni hali inayochangia kushusha taaluma mashuleni.