RC Dar asema wamejipanga kukabiliana na mgomo wa madaktari

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick

Na Magreth Kinabo – MAELEZO

SERIKALI imesema imejipanga vizuri ili kukabiliana na mgomo wa madaktari unaoendelea katika baadhi ya hospitali za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama kwa madaktari wanaoendelea na kazi walitishiwa maisha.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alipokuwa katika maadhimisho wa Siku ya Wanawake Duniani yaliyo fanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini hapa, ambapo amesema imezijengea uwezo hospitali za Wilaya ili ziweze kutoa huduma.

Mbali na hilo imesema kuwa imehakikisha vipimo vinakuwepo mfano x-ray, hivyo mgomo huo hautatishia maisha ya Watanzania. “Tutaendelea kuhakikisha madaktari wanaonendelea kutoa huduma kwenye hospitali za wilaya kwa kesi zinazoshindikana tutawaelekeza nini cha kufanya ili wawaweze kuwapeleka wagonjwa katika hospitali zingine hata kwa gharama za Serikali.

“Wapo madaktari walioonyesha moyo wa uzalendo kwa kuendelea kutoa huduma katika hospitali za Mwananyamala…na katika vituo vya afya ninawapongeza kwa kutii na kuheshimu kauli ya Waziri Mkuu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari bila kugoma ambapo wamendelea kuokoa maisha ya ndugu zao na Watanzania. Naomba waendelee na utaratibu huo,” alisema Sadick.

Aliwataka madaktari hao kuendelea kupokea wagonjwa na wananchi wasiogope kuwapeleka wagonjwa wao kwenye hospitali na vituo vya afya vinavyoendelea kutoa huduma.
Akizumgumzia kuhusu tatizo la baadhi ya madakatri wanaoendelea na huduma kutisha kwa kuandikiwa ujumbe kwa njia ya simu alisema serikali itaendelea kuwalinda kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama ili waendelee kutoa huduma kwa usalama wa maisha yao. “Tutatumia ulinzi wa aina yeyote si lazima uwe wa kutumia sare maalum,” alisisitiza.

Wakatihuohuo Mkuu wa mkoa Sadick alitumia nafasi hiyo kuwaeleza Watanzania kwamba leo, Rais Jakaya Kikwete atalihutubia Taifa kwa njia ya redio na televisheni kupitia wazee wa Jiji la Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Diamond kuanzia saa 10:00 jioni.