Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amewataka viongozi wa Serikali mkoani hapa ngazi zote, kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari.
Mulongo alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali
kutokutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pale wanapohitaji
taarifa jamabo ambalo linasababisha wananchi kutokufahamu namna
Serikali inavyotejekeza wajibu na mujukumu yake.
Mkuu huyo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akifungua mkutano maalum wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani
Arusha (APC), uliofanyika katika Hoteli ya Briston.
Alisema kuwa Serikali mkoani hapa kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya
habari katika kukuza maendeleo, kwa kuzingatia Katiba wa kutoa habari itahakikisha kuwa pindi taarifa zinapohitajika watatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari.
“Nitawakutanisha na wakuu wa idara mbalimbali mkoani hapa ili muweze
kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha tunashirikiana na ninyi
ili kuweza kujenga na kuimarisha amani na maendeleo ya wananchi bila
kuandika habari za uchochezi na zile zenye upotoshaji kwa jamii, mnatakiwa kuzingatia maadili ya taaluma yenu,” aliongeza Mkuu huyo
Aidha Mulongo aliwatahadharisha wamiliki wa vyombo vya habari
kutokuingilia taaluma ya habari na kuiacha ijitegemee ili taaluma hiyo iweze kuthaminiwa kama taaluma nyingine katika ustawi wa taifa.
Aliwaasa waandishi kufanya kazi kwa juhudi ikiwa ni pamoja na kuibua miradi itakayowawezesha kujiletea maendeleo ya kiuchumi sambamba na kujiunga na kilabu ili kuwa na ushirikiano katika kazi zao na kubadilishana uzoefu.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya
katiba ya Klabu hiyo pamoja na wanachama kusomewa mapato na matumizi
ya mwaka 2011-2012.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa klabu ya waandishi
habari mkoani hapa Claud Gwandu alisema kuwa serikalini kumekuwa na
tatizo la urasimu katika utoaji wa taarifa kwa waandishi kwa kutoa
habari za kujisifia tu,bila kutoa habari za maendeleo ya wananchi.