Na Joachim Mushi
Bukoba
MKUU wa Mkoa wa Bukoba, Mohamed Babu ameliomba Shirika la Hifadhi ya Jamii la Taifa (NSSF) kuwekeza zaidi katika mkoa huo kwani kwa sasa kuna miundombinu ya kuvutia wawekezaji tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Babu aliyasema hayo juzi alipotembelewa na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo ililofanya ziara katika mkoa huo kutembelea miradi inayoendeshwa na NSSF pamoja na ile inayoshiri katika namna moja kuiendeleza ikiwemo kutoa mikopo.
NSSF kwa sasa imejenga jengo kubwa na la kisasa la ghorofa nne lililopo Bukoba mjini kwa jili ya kupangisha wawekezaji ofisi mbalimbali pamoja na shughuli nyingine, na pia ndiyo waliotoa mkopo kwa mwekezaji wa kiwanda cha Sukari Kagera.
Akizungumza na wajumbe hao ofisini kwake, Babu alisema Mkoa wa Bukoba kwa sasa unaingilika kwa njia zote kiusafiri; yaani kwa barabara, njia ya ndege na maji mazingira ambayo yanavutia kiuwekezaji tofauti na miaka ya nyuma.
Akifafanua zaidi alisema nishati ya umeme inayopatikana katika mkoa wake ni ya uhakika tofauti na mikoa mingine, kwani hata adha ya mgawo wa umeme unaoendelea nchini haiwaathiri kutokana na wao kutumia nishati hiyo kutoka nchini Uganda .
Aidha akizungumzia miradi ya uwekezaji ya NSSF iliyopo mkoani hapo ikiwemo jengo jipya na la kisasa; alisema Mkoa wa Bukoba bado unakuwa jambo ambalo linahitaji ofisi za kutosha hivyo kujengwa kwa jengo hilo lenye ofisi nyingi limewasaidia wawekezaji.
“Jengo hili limetusaidia ofisi maana mkoa wetu ni mji ambao bado unakuwa bila jengo lile hali ingekuwa mbaya zaidi…tunayo maeneo mengi hapa Bukoba, watu wanaongezeka kila uchao , tunahitaji nyumba na tunavyo viwanja elfu tano (5,000) mnaweza kutusaidia uwekezaji eneo hili.
Hata hivyo aliishukuru bodi hiyo kwa ufadhili wa mkopo inayoufanya kwa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, kwani kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya mkoa hasa kibiashara kutokana na mchango wake.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF, Abubakar Rajab akimjibu Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya shirika hilo alikiri Bukoba kuwa sehemu nzuri kiuwekezaji na nafasi yoyote itakayojitokeza watatoa kipaumbele katika mkoa huo. Mkoa wa Kagera una majengo manne ambayo NSSF imewekeza.
“Hapa ni mahali pazuri kwa uwekezaji fursa yoyote itakayo jitokeza, tayari taarifa tunazo…tunapokea hilo ,” alisema Mwenyekiti huyo.