Rambirambi Msiba wa Makamu wa Rais FIFA

FIFA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shrikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter kutokana na kifo cha makamu wake mwandamizi Julio Grondora.

Amesema yeye binafsi na jamii ya mpira wa miguu Tanzania kwa ujumla wanaomboleza msiba wa Grondora ambaye pia alikuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Argentina (AFA).

Ameongeza kuwa Grondora alikuwa mtumishi mwandamizi wa mpira wa miguu, kwani alijitoa katika kuutumikia mpira wa miguu, na mchango wake katika maendeleo ya mchezo huo utaendelea kukumbukwa wakati wote.

Rais Malinzi amesema familia ya mpira wa miguu nchini Argentina imepata pigo, na ametoa pole kwa familia ya marehemu, AFA na familia nzima ya FIFA na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina.

KLABU VPL, FDL ZATAKIWA KUWASILISHA MABENCHI YA UFUNDI

Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinatakiwa kuwasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) orodha ya watendaji wa mabenchi yao ya ufundi yakiongozwa na Kocha Mkuu.

Ni wajibu wa klabu kuhakikisha zinatekeleza maagizo hayo kwani ni matakwa ya Kanuni za VPL na zile za FDL.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itaanza kutimua vumbi Septemba 20 mwaka huu wakati ile ya FDL inatarajia kuanza Oktoba mwaka huu.

AZAM KUCHEZA MICHUANO YA KAGAME

Azam FC ndiyo itakayoiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliyopangwa kuanza Agosti 8 mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiteua Azam kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano hiyo baada ya waandaaji wake, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuamua kuindoa Yanga iliyokuwa icheze awali.

CECAFA imesema baada ya majadiliano na Yanga kupitia TFF, klabu hiyo ilipewa muda hadi jana (Agosti 4 mwaka huu) iwe imetekeleza matakwa ya kikanuni ili iruhusiwe kushiriki michuano hiyo lakini haikufanya hivyo.

Yanga iliwasilisha orodha ya wachezaji wengi wa kikosi cha pili kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo, jambo ambalo limekatawaliwa na CECAFA kwa vile linakwenda kinyume na kanuni za michuano hiyo.

Azam FC ambayo ilishika nafasi ya pili- nyuma ya Yanga katika ligi iliyopita msimu wa 2012/2013 imekubali kushiriki michuano hiyo na inatarajia kuondoka nchini kesho (Agosti 6 mwaka huu) kwenda Kigali.

Msafara wa Azam FC katika michuano hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, James Mhagama.