RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mwandishi wa Habari na Msanifu wa Habari Msaidizi Mkuu wa Gazeti la Uhuru, Dunia Mzobora, kilichotokea tarehe 27 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya shinikizo la damu.
Marehemu aliajiriwa katika Magazeti ya Uhuru na Mzalendo mwaka 1989 kama Mwandishi wa Habari Mwanafunzi, kisha akaendelea kupanda ngazi hadi kufikia cheo cha Msanifu wa Habari na hatimaye kuwa Msanifu Mkuu Msaidizi, cheo alichokuwa akikishikilia hadi mauti yalipomkuta.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa Waandishi wa Habari Shupavu na Mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU, kilichosababishwa na ugonjwa wa shinikizo la damu baada ya kuwa amepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete.
Rais Kikwete amesema binafsi alimfahamu vyema Marehemu Dunia Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma vilivyo katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa kutumia vyema kalamu yake, na kwa kuzingatia kikamilifu Maadili ya Taaluma yake ya Uandishi wa Habari.
“Kufuatia taarifa za kifo cha Dunia Mzobora, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara na Wafanyakazi wote wa Kampuni ya Magazeti ya Chama ya Uhuru na Mzalendo na kwa kweli Waandishi wote wa Habari nchini, Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Waandishi wa Habari Mahiri ambaye amelitumikia vyema Taifa lake kupitia Tasnia ya Habari”.
“Aidha kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza Baba, Kiongozi na Mhimili wa Familia”.
Rais Kikwete amewahakikishia Wanafamilia kuwa yeye binafsi yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Dunia Mzobora, Amina.
Rais Kikwete amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu aliyekuwa kiungo cha Familia yao, kwani yote ni Mapenzi yake Mola.