RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameitumia familia ya Mzee James Irenge salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mzee huyo ambaye katika uhai wake alimfundisha Baba wa Taifa, hayati Julius K. Nyerere katika Shule ya Msingi ya Mwisenge.
Mzee Irenge ambaye alimfundisha Julius Kambarage Nyerere katika darasa la kwanza na la pili, alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwake mjini Musoma kwa matatizo ya moyo akiwa na umri mkubwa.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Mzee James Irenge. Historia yake ya kumfundisha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni dhahiri imechangia katika historia ya jumla ya nchi yetu kujitafutia uhuru, na hatimaye kujitawala kwa sababu ya mchango wa Mwalimu Nyerere. Mzee ametuaga lakini mchango wake utabakia katika historia ya nchi yetu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda kuwatumieni nyie wana-familia ya Mzee Irenge salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa wa mhimili wa familia. Napenda kuwajulisheni kuwa niko nanyi katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Marehemu James Irenge, Amen.”