Reinhard Grindel amechaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la Kandanda la Ujerumani – DFB, na kupewa jukumu la kurejesha uaminifu kufuatia kashfa iliyotokana na malipo ya kutatanisha kabla ya Kombe la Dunia la 2006
Grindel mwenye umri wa miaka 54, alikuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo. Anachukua nafasi ya Wolfgang Niersbach, aliyejiuzulu mwezi Novemba wakati kashfa hiyo ilianza kufichuka. Grindel, mwanasiasa wa kihafidhina, alikuwa mweka hazina wa DFB.
Shirikisho hilo la kandanda lenye ushawishi mkubwa lilitikisika kabisa kutokana na kashfa hiyo iliyozunguka dimba la Kombe la Dunia la mwaka wa 2006 nchini Ujerumani.
Uchunguzi wa kampuni moja ya sheria haukupata ushahidi wa kununuliwa kura kabla ya dimba hilo, ijapokuwa haikufutilia mbali suala hilo.
Ripoti hiyo iligundua kuwa DFB iliipa Qatar zaidi ya dola milioni 10 malipo ambayo hayakueleweka. Franz Beckenbauer na maafisa wengine wakuu wa Kombe la Dunia la 2006 wanafanyiwa uchunguzi na kamati ya maadili ya FIFA.