Rais Wade wa Senegal kugombea urais tena

Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade

MAHAKAMA Kuu ya Senegal imetupilia mbali kesi ya rufaa ya vyama vya upinzani na kuamua kuwa Rais Abdoulaye Wade anaweza kugombea tena kiti cha urais wa nchi hiyo kwa mara ya tatu.

Upinzani umesema Katiba ya nchi hiyo imeweka kikomo cha mihula miwili, lakini mahakama hiyo imesema, Wade hafungwi na sheria hiyo kwa sababu, sheria hiyo ilipitishwa akiwa katika muhula wake wa kwanza.

Uamuzi wa kumruhusu, Wade kugombea kwa muhula wa tatu umezua maandamano nchini Senegal. Wasiwasi bado umetanda nchini Senegal baada ya ghasia zilizozuka Ijumaa usiku kufuatia tangazo kwamba Rais Abdoulaye Wade atawania urais kwa mara ya tatu .

Baraza la Kikatiba nchini humo lilimwiidhinisha, Wade, ambaye ana miaka 85, kugombea urais kwa muhula wa tatu lakini ikatupilia mbali ule wa mwanamuziki Youssou N’dour ikisema hakuwa na saini 100,000 zilizokuwa zinahitajika.

Wanaompinga Rais Wade wanasema katiba inaeleza wazi kwamba kiongozi hafai kuwania urais kwa zaidi ya mihula miwili. Lakini Wade na wanaomuunga mkono wanasema katiba ilibadilishwa baada ya uchaguzi wa urais na hivyo sheria ya kuwania urais mara mbili tu haimfungi kwa njia yote ile. Anasema sheria hii itatekelezwa kwa marais watakaofuatia.

Wapinzani wake Rais Wade wanasema hajafanya lolote kukabiliana na umaskini katika miaka 12 ambayo ametawala Senegal, ambako kazi hazipatikani kwa urahisi. Pia wanasema kwamba hajakuwa na bidii katika kukabiliana na ufisadi.

Hata hivyo, Rais Wade amejitetea akisema kwamba chini ya utawala wake, matumizi ya elimu yameongezeka na miundombinu kama vile barabara kujengwa. Anasema hii ni ishara kwamba amefanya juhudi kuhakikisha kwamba Senegal ni kitovu cha biashara.
-BBC