Rais wa Zamani wa Ujerumani Atoa Changamoto Kuhusu Wajasiriamali EAC

RAIS wa zamani wa Ujerumani, Horst Kohler

Na Nicodemus Ikonko, EANA

RAIS wa zamani wa Ujerumani, Horst Kohler amepania kutoa msukumo wa kuendeleza ujasiliamali Mdogo na wa Kati (SMEs) kwa Afrika Mashariki, ambao unategemewa karibu na asilimia 70 za biashara zinazochipukia hivi sasa katika kanda hiyo.

Katika mkutano, kati yake na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera, Berling, Ujerumani mwishoni mwa wiki, kiongozi huyo wa zamani wa Ujerumani pia ameahidi kuhamasisha uwekezaji na wajasiliamali wa Ujerumani kuwekeza EAC ili kukuza ujasiliamali mdogo na wakati.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC na Shirika la Habari Huru la Afrika Mashariki (EANA) kupata nakala yake, Rais huyo wa zamani ameupongeza mtangamano wa EAC wenye wanachama watano akisema njia hiyo ndiyo bora zaidi katika mapambano dhidi ya umasiki na kujiletea maendeleo. Wanachama wa EAC ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Kwa upande wake Dk. Sezibera alitumia nafasi hiyo kumweleza Rais huyo wa zamani juu ya ziara anayoendelea nayo mjini Berling na majadiliano muhimu anayoendelea kufanya na maafisa mbalimbali waandamizi wa serikali ya Ujerumani.

Alitoa wito kwa wajasiliamali wadogo na wa kati wa Ujerumani kuwa na moyo wa kuwekeza katika kanda ya Afrika Mashariki. “Ziara yangu hapa inajikita zaidi katika kuimarisha mashikamano wetu wa kiuchumi na kihistoria,” alifafanua Dk. Sezibera.

Alimshukuru Rais Kohler kwa kuwezesha upatikanaji wa sehemu ya Euro milioni 14 zilizotumika katika kufanikisha ujenzi wa ofisi za makoa makuu ya EAC, mjini Arusha, Tanzania. Ofisi hizo zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Novemba 28, 2012.

Dk. Sezibera yupo nchini Ujerumani pamoja na mambo mengine kushiriki katika Jukwaa la Kwanza la Biashara kati ya Ujerumani na EAC ambalo linalenga kuvutia wawekezaji zaidi kutumia nafasi zilizopo EAC kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.