RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans, Yusuf Manji kufuatia timu yake kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2014/2015.
Katika salamu zake za pongezi, Malinzi amesema kutwaa Ubingwa wa VPL ni jambo muhimu na sasa wanapaswa kuanza maaandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa barani Afrika mwakani. Klabu ya Young Africans imetwaa Ubingwa wa Ligi Kuu nchini kwa mara ya 25 (ishirini na tano) jana, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya Polisi Morogoro katika uwanja wa Taifa huku ikiwa na michezo miwili mikononi kabla ya ligi kumalizika.
Waziri wa Habari, Vijana Utamuduni na Michezo, Dr. Fennela Mkangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kukabidhi Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Mei 6, 2015 katika mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Young Africans.
VILABU VPL VYAPIGWA FAINI, WAAMUZI WAFUNGIWA
Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 149 dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga
Pia Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa timu ya Polisi Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.
Naye Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa kwenye benchi la Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi msaidizi namba moja Martin Mwalyanje. Suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Kipa wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumkanyanga na kutaka kumpiga mwamuzi Eric Onoka kwenye mechi namba 155 dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Kabla ya kufanya kitendo hicho alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu.
Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es Salaam.
Naye Kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi na kuwatolea lugha ya matusi mazito ya nguoni baada ya mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5)(c) ya Ligi Kuu.
Mwamuzi wa mechi kati ya Azam FC na Kagera Sugar, Stephen Makuka na mwamuzi msaidizi namba mbili Said Mnonga wameondolewa kwenye orodha za waamuzi wa Ligi Kuu na kufungiwa miezi 12 kwa kushindwa kumudu mchezo kwa uzembe. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.
Pia Kamishna wa mechi hiyo Bevin Kapufi amefungiwa mwaka mmoja kwa kutoa taarifa isiyo sahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu. Naye Kamishna wa mechi namba 159 kati ya Mbeya City na Simba, Joseph Mapunda amepewa onyo kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 159 dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Pia Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mechi (technical meeting) dhidi ya Ruvu Shooting. Mechi hiyo namba 161 ilichezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(2)(a) ya Ligi Kuu.
LIGI YA MABINGWA WA MIKOA SASA MEI 9
Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) sasa itaanza Jumamosi Mei 9, 2015 badala ya Jumamosi Mei 2, 2015 kama ilivyokua imetangazwa awali.
Uamuzi huo umefanyika ili kutoa fursa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kukamilisha maandalizi ya mwisho ikiwemo ukaguzi wa viwanja ambavyo vitatumika katika RCL na masuala mengine ya kumsingi.
Tunaomba radhi kwa usumbufu ambao utakuwa umejitokeza kutokana na taarifa hii ya kusogeza mbele kuanza kwa ligi, lakni pia kuzitakia kila la kheri timu zinazoshiriki katika maandalizi yao.
Ratiba ya mashindano itatolewa/kutumwa leo kama ilivyopangwa awali.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)