SIMBA SC imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation baada ya kuifunga SIngida United mabao 5-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo uliochezeshwa na refa Mwanahamisi Matiku wa Dar es Salaam, mabao ya Simba SC yamefungwa na Awadh Juma, Hamisi Kiiza kila mmoja mawili na lingine Danny Lyanga, wakati la Singida limefungwa na Paulo Malamla.
Lyanga ndiye aliyekata utepe wa mabao hii leo Uwanja wa Taifa dakika ya tatu baada ya kuuwahi mpira uliookolewa na beki wa Singida, Kennedy Juma kufuatia krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Kiiza ‘Diego wa Kampala’ akaifungia Simba bao la pili dakika ya 19, akimchambua kipa Jackton Munna kufuatia krosi ya Tshabalala tena.
Kiiza akafunga bao la tatu dakika ya 66 na la 18 msimu huu tangu ajiunge na Simba kwa kichwa akimalizia krosi ya Mganda mwenzake, Brian Majwega.
Kiungo fundi na asiye na mambo mengi, Awadh Juma Issa ‘Mwana Zanzibar’ akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 83, baada ya krosi ya Mrundi Emery Nimubona.
Awadh akakamilisha sherehe za mabao za Simba kwa kufunga bao la tano dakika ya 86 akimalizia krosi ya nyota wa mchezo wa leo, Tshabalala wa Manzese.
Mchezo mwingine wa Kombe la TFF leo, Geita Gold inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Simba, Suleiman Matola imeitoa Toto Africans baada kwa kuichapa 1-0, bao pekee la Chibuga Chibuga ‘Balotelli’ Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Geita na Simba zinaungana na Yanga iliyoitoa JKT Mlale kwa kuifunga 2-1 Februari 24, Ndanda FC iliyowatoa waliokuwa wanashikilia taji, JKT Ruvu kwa kuwafunga 3-0, Coastal Union iliyoifunga 1-0 Mtibwa Sugar juzi, Prisons iliyowafunga 2-1 Mbeya City na Mwadui iliyowafunga 3-1 Rhino Rangers.
MATOKEO NA RATIBA 16 BORA KOMBE LA TFF
Leo; Februari 28, 2016
Simba SC 5-1 Singida United (Taifa, Dar es Salaam)
Toto African 0-1 Geita Gold (Kirumba, Mwanza))
Februari 24, 2016
Yanga SC 2-1 JKT Mlale (Taifa, Dar es Salaam)
Februari 26, 2016
Ndanda FC 3-0 JKT Ruvu (Nangwanda, Mtwara)
Coastal Union 1-0 Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga)
Februari 27, 2016
Mwadui FC 3-1 Rhino Rangers (Mwadui, Shinyanga)
Prisons 2-1 Mbeya City (Sokoine, Mbeya)
Kesho; Februari 29, 2016
Panone FC Vs Azam FC (Ushirika, Moshi)