Rais wa China Kuzinduwa Ukumbi wa Mwalimu J. Nyerere

Rais wa China Xi Jinping

Hassan Silayo-Maelezo

RAIS wa China, Xi Jinping anatarajia kufungua Jengo la Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa la Julius Nyerere Convertion Centre lililopo jijini Dar-es-Salaam linalomilikiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa ziara yake nchini inayotarajia kuanza mwanzoni mwa wiki ijayo.

Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo John Haule wakati wa ziara ya kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walipotembelea jengo hilo ili kuona maendeleo ya ujenzi. Haule alisema kuwa ujenzi wa ukumbi huo ni matunda ya mahusiano mazuri ya ushirikiano yaliyopo baina ya Serikali ya China na ya Tanzania kwa makubaliano maalum ikiwa ni kama msaada na mkopo nafuu usio na riba ambao utalipwa kwa awamu mbili tofauti.

“Ukumbi huu ni wa kisasa, utatumika kama sekta ya utalii na biashara utasaidia kuliingizia Taifa fedha za kigeni kwani una sehemu kubwa ya kuegesha magari 222, chumba cha habari, mgahawa, ofisi za wazi na maktaba ndogo”, alisema Haule. Aidha Haule alisema kuwa ziara ya Rais Xi Jinping ni kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na China na kueneza sera ya mambo ya nje kwa kipindi chote cha utawala wake atakachokuwa madarakani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mbunge wa Monduli Edward lowassa alisisitiza umuhimu wa utunzanji wa jengo hilo na kukamilisha mapema vitu ambavyo havijakamilika ili viweze kufanyiwa kazi kabla ya ufunguzi. Ujenzi wa ukumbi huo wenye ghorofa tatu na kumbi nne za mikutano zenye uwezo kupokea washiriki zaidi ya 1800 ulianza mwaka 2009 na umegharimu dola za kimarekani milioni 29.7.