Rais: Tutaendelea Kukopa kwa Maendeleo Yetu

Tanzania itaendelea kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo kwa sababu uwiano wa deni la nje na pato la taifa bado ni mdogo na mikopo inayotafutwa ni ile yenye masharti nafuu.

Ili mradi mikopo iwe ya masharti nafuu na yenye manufaa
kwa wananchi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania itaendelea kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo kwa sababu uwiano wa deni la nje na pato la taifa bado ni mdogo na mikopo inayotafutwa ni ile yenye masharti nafuu.

Aidha, Rais amesema kuwa hakuna nchi duniani imeendelea bila kukopa na wanaosambaza uongo kuwa deni la Tanzania ni kubwa kiasi cha kushindwa kubebeka wanashiriki siasa za kuwadanganya na kuwababaisha wananchi bila sababu za msingi.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali wakati alipozungumza jana, Jumatatu, Machi 18, 2013, katika sherehe ya kuzindua Taasisi ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Tanzania (VETA) iliyoko Kipawa, Dar es Salaam, moja ya vyuo 27 vya VETA nchini.
Rais Kikwete amezindua Taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya shughuli nyingi kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Miongoni mwa shughuli nyingine muhimu alizozifanya jana ni kuweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Awamu ya Tatu ya Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa na Ajali Muhimbili (MOI) na pia kuzindua maabara ya kisasa ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwenye Makao Makuu ya Mamlaka hiyo katika eneo la Mabibo.

Jengo la Awamu ya Tatu ya Taasisi ya MOI linajengwa kwa gharama kubwa ya Sh. Bilioni 17.9 (17, 969,680,000) ambazo zinatolewa kama mkopo na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkopo unaodhaminiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya Sera ya Uwekezaji ya Mfuko inayolenga kuboresha Sekta ya Afya nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua Taasisi hiyo ya VETA ambayo imegharimu jumla ya Sh. Bilioni tatu zikiwamo Bilioni 1.8 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea, Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwashangaa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiendesha kampeni inayodai kuwa Serikali ya Tanzania imekopa sana kutoka nje.
Mbali na Jamhuri ya Korea, Serikali ya Tanzania imechangia kiasi cha Sh. Bilioni 1.2 katika mradi huo ambao ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa vyuo vya kisasa vya VETA ambavyo vimejengwa katika mikoa ya Lindi, Pwani, Manyara na Katavi kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Jamhuri ya Korea.
Kipawa Veta ni chuo pekee kinachotoa mafunzo ya ICT miongoni mwa vyuo vyote vya VETA nchini na Serikali ya Tanzania, nchi ambayo watoto wake 800,000 wanamaliza shule za msingi kila mwaka, inatafuta fedha za kujenga vyuo vya VETA katika mikoa mpya ambayo haijapata vyuo hivyo – Geita, Simiyu, Njombe na Rukwa ambao chuo chake kimekwenda mkoa mpya wa Katavi.
Aidha, Serikali inakusudia kujenga vyuo zaidi vya VETA katika wilaya za Ukerewe, Kilindi, Namtumbo, Ludewa na Chunya.
Rais Kikwete amewaambia wananchi kuwa ni jambo la kushangaza kuwa wapo baadhi ya watu wanaoshinda wanaeneza siasa kuwa Tanzania inakopa ama imekopa sana.
“Kwanza sisi tunakopa kidogo sana kulinganisha na pato letu la taifa. Pili, hakuna nchi duniani isiyokopa kwa maendeleo yake. Tatu, ukopaji wa Tanzania unaongozwa na misingi maalum na uko chini ya Kamati Maalum ya Madeni ambayo huchunguza kila uamuzi wa Tanzania kutaka kukopa.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Misingi mikubwa ya ukopaji wa Tanzania ni kwamba lazima mkopo uwe wa masharti nafuu – concessionary loans –ikiwa yenye riba ya chini, muda mrefu wa kujiandaa kulipa mkopo na muda mrefu zaidi wa kulipa. Chukulia mfano wa Daraja la Mto Malagarasi (Daraja la Kikwete) Mkoani Kigoma. Deni ni bilioni tatu, riba yake ni asilimia 0.02, muda wa kujiandaa kulipa ni miaka 10 na muda wenyewe wa kulipa ni miaka 40. Sasa kuna mkopo rahisi zaidi kuliko huu?”.
Rais Kikwete ameongeza: “Hawa watu, wengine wasomi wazuri, wanashinda wanazunguka wakidai kuwa Watanzania tunadaiwa sana, eti kila mtu anadaiwa Sh. 400,000 na kwamba tutalipa fedha hizo kwa miaka 50 ijayo. Laki nne zitakuwa sijui kiasi gani katika miaka 50 ijayo? Wanachotaka watu hawa ni Serikali isifanye kitu, na sisi katika Serikali hatukubali. Tutaendelea kuwapuuza na kuzidisha jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo. Tutakopa kama tunadhani mkopo utachangia maendeleo yetu.”
Ametoa mfano wa barabara ya Dar es Salaam – Morogoro iliyojengwa na Waingereza. “Mkopo wa ile barabara ulitolewa mwaka 1956 baada ya Serikali ya Uingereza kupata fedha hizo New Zealand. Mkopo ule tunalipa sisi sasa, miaka 56 baadaye.”
Amesema Rais Kikwete: “Wananchi nataka kuwahakikishieni kuwa tutaendelea kukopa kwa busara kama ambavyo tumekuwa tunafanya miaka yote. Hawa wenyewe wanakopa kuendesha shughuli zao binafsi lakini wanatushutumu sisi kwa kukopa kuleta maendeleo ya nchi yetu. Wasiwababaisheni ndugu wananchi watu hawa. Msitishwe na maneno yao ya siasa.”