Na Salva Rweyemamu
Tanzania imeombwa kuisaidia Gabon kubuni, kuanzisha na kusimamia mitaala inayofaa kuanzisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za nchi hiyo kufuatia uamuzi wa Serikali ya Gabon kuanza kufundisha lugha hiyo tokea elimu ya msingi.
Aidha, Rais wa Gabon, Mheshimiwa Ali Bongo Ondimba amemwomba binafsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho kusaidia kumpatia mwalimu binafsi wa kumfundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada zake za kuonyesha mfano wa kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wananchi wake.
Maombi hayo mawili ya Serikali ya Gabon yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika usiku wa Ijumaa, Julai Mosi, 2011, kwenye Ukumbi wa Kijiji cha AU cha Sipopo, nje kidogo ya mji mkuu wa Equatorial Guinea wa Malabo, ulioko katika Kisiwani cha Bioko.
Viongozi hao wawili, Rais Kikwete na Rais Ondimba walihudhuria Mkutano huo wa siku mbili na Rais Kikwete amekubali maombi hayo ambayo yanathibitisha utekelezaji wa azma yake ya kueneza lugha ya Kiswahili katika Afrika na duniani pote ambayo aliitangaza tokea mwanzoni mwa Urais wake mwishoni mwa 2005.
Gabon inakuwa nchi ya kwanza katika Afrika kukumbatia na kuamua kufundisha Kiswahili mashuleni nje ya nchi za Jumuia ya Mashariki za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda hata kama lugha ya Kiswahili inazungumza na mamilioni ya watu nje ya eneo la Jumuia hiyo ndani na nje ya Afrika.
Kiswahili ni moja ya lugha kuu zinazotumiwa kwa shughuli za mawasiliano katika Umoja wa Afrika na wakati anakubali kuwa Mwenyekiti wa Umoja huo Januari 31, 2008 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete alitoa hotuba yake ya kukubali nafasi hiyo kwa lugha ya Kiswahili, hatua iliyomjegea sifa kubwa miongoni mwa viongozi wenzake na Waafrika wengine.
AU inazitambua lugha zote za Waafrika kuwa ni lugha rasmi za Bara la Afrika lakini katika shughuli zake za mawasiliano Umoja huo hutumia lugha sita ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno na Kihispania.
Mara baada ya kupokea maombi hayo, Rais Kikwete alimkabidhi jukumu la kufanikisha utekelezaji wa maombi hayo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi, ambaye alikuwa kwenye ujumbe wa msafara wa Mheshimiwa Rais Kikwete kwa ajili ya mkutano huo wa Malabo.
Rais Kikwete ambaye alirejea nchini jioni ya jana, Jumamosi, Julai 2, 2011, leo, Jumapili, Julai 3, 2011, ameanza ziara fupi za mikoa ya Kagera na kigoma.
Ends