SERIKALI ya Malawi, haitakuwa mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Afrika uliotarajiwa kufanyika mjini Lilongwe mwezi Ujao.
Hatua hii imekuja baada ya malumbano kuhusu rais wa Sudan Omar El Bashir anayetakiwa na mahakama ya ICC kwa makosa ya Jinai ikiwa aruhusiwe au asiruhusiwa kuhudhuria mkutano huo.
Umoja wa Afrika ulikuwa umesisitiza kuwa lazima Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, aalikwe.
Muungano wa Afrika imekuwa ikitaka kibali cha kukamatwa kwa Bashir kutupiliwa mbali na kuisisitizia Malawi kumkaribisha rais Bashir.
“Licha ya kuwa tuna wajibu kwa AU lakini pia tuna tunawajibika kwa taasisi zingine,” alisema makamu wa rais wa Malawi.
Rais wa zamani wa nchi hiyo,Bingu wa Mutharika, aliyefariki mwezi Aprili, alipinga wito wa kukamatwa kwa rais Bashir.
Tangu kifo chake, mrithi wake rais Joyce Banda amechukua hatua za kuwafurahisha zaidi wahisani wake kwa kufanya mageuzi kadhaa.
Mnamo Alhamisi, Sudan iliitaka Muungano wa Afrika, kuhamisha mkutano huo hadi katika makao makuu ya Muungano wa Afrika baada ya Malawi kusema kuwa Bashir hakaribishwi katika taifa hilo la Ukanda wa Afrika Kusini.
Kulingana na mkataba wa ICC, nchi wanchama waliosaini mkataba huo wana wajibu wa kuwakamata watu wanaotakikana na mahakama hiyo.
” Baada ya kutafakari maslahi ya wananchi wa Malawi, nataka kuwajulisha Wamalawi, kuwa baraza la mawaziri lilikutana leo na kuamua kua Malawi haina haja ya kuitikia masharti ya Muungano wa Afrika, na kwa hivyo haitakuwa mwenyeji wa mkutano.” shirika la AFP lilimnukuu makamu wa rais Kumbo Kachali akiongea na waandishi wa habari.
Wakati rais wa zamani Mutharika alipokataa kuitikia wito wa kumkamata rais Bashir wakati alipozuru Malawi mwezi Oktoba mwaka jana, mahakama ya ICC iliwasilisha malalamiko kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Rais Bashir ndiye rais wa kwanza aliye mamlakani kutolewa kibali cha kukamatwa mahakama ya ICC ambayo ilimshtaki kwa tuhuma za mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.
-BBC