Rais Obama Aomba Bunge Kuidhinisha Vita, Mandela Atoka Hospitali Akiwa Mahututi

Rais wa Marekani, Barack Obama

HAIKUSADIKIKA kuwa Marekani itachukua hatua za haraka za kijeshi dhidi ya Syria, baada ya Rais Barack Obama wa nchi hiyo kuliomba bunge lake kuidhinisha shambulio. Kwa sasa Bunge halitaanza tena vikao vyake hadi Septemba 9, 2013.

Mswada huo uliowasilishwa unaomba idhini ya bunge kutumia nguvu kuizuia serikali ya Syria kutumia silaha za kemikali kwenye mashambulio. Kuchelewa kwa ratiba ya Marekani piya kunawapa muda wakaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa kumaliza uchunguzi ndani ya maabara.

Wakaguzi hao wamerudi na sampuli walizopata kwenye eneo linalodaiwa kuwa lilishambuliwa kwa silaha za kemikali, karibu na Damascus.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma


Wakati huo huo, Serikali ya Afrika Kusini inasema kuwa rais wa zamani, Nelson Mandela, ametolewa hospitali ambako amekuwa akitibiwa mapafu tangu mwezi Juni. Hata hivyo taarifa katika tovuti ya rais wa Afrika Kusini inasema kuwa Mandela bado ni mahtuti na hali yake wakati mwengine inabadilika.

Lakini madaktari wake wanaamini akiwa nyumbani kwake mjini Johannesburg atapata matibabu sawa na yale ya hospitali. Nyumba ya Mandela imebadilishwa ili kumruhusu kupata matibabu ya mgonjwa mahtuti akiwa nyumbani. Serikali imesema inamtakia mema wakati akiendelea na matibabu.

-BBC