RAIS wa Tanzania Mh. Dk John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani(WPFD) inayotarajia kufanyika mkoani Mwanza. Maadhimisho hayo ya siku mbili yaani Mei 2 na 3, 2017 yanatarajia kuwakutanisha wanataaluma ya habari na wadau anuai wa vyombo vya habari kujadili masuala mbalimbali ya tasnia ya habari.
Wakizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa pamoja na vyombo vya habari uliyoshirikisha wadau mbalimbali walioshiriki kufanikisha maandalizi hayo, walisema maadhimisho ya WPFD kitaifa yanafanyika mkoani Mwanza na yatafunguliwa na mgeni rasmi, Rais Dk. John Magufuli pamoja na Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Wasanii.
Akizungumza na wanahabari, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-Tanzania, Salome Kitomari ambao ni waratibu wa maadhimisho hayo, alisema Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari yanayotarajia kufanyika yanabeba maana kubwa kwa wanahabari na wadau wa vyombo vya Habari Duniani kutokana na umuhimu wa tasnia yenyewe.
Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kwani hakuna taifa linazoweza kuendelea na kuwa na ustawi bila ya uhuru wa vyombo vya habari. Alisema vyombo vya habari ndivyo vinavyotoa mchango wa kuibua uozo na hata kuleta uwajibikaji maeneo mbalimbali ambapo serikali nayo uweza kuchukua hatua.
Alisema wanahabari hawana budu kufanya kazi kwa uhuru huku wakizingatia sheria na kujali usalama wao katika utendaji wa kazi ili kuepuka madhara yanayoweza kuhatarisha usalama wa wanahabari. “Wanahabari waliofanikiwa kupata mafunzo ya usalama kazini wayatumie vizuri ili kuepuka madhara maana yakitumika vizuri yanasaidia,” alisema Bi. Kitomari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga alivitaka vyombo vya habari kubadilika na kuanza kujipangia vipaombele vya kufanya kazi na kuacha utaratibu wa kufanya kazi kwa kufuata mkumbo wa matukio. Alisema umefika wakati vyombo vya habari kujipangia agenda za kuzifanyia kazi na kuacha kuwasubiri wanasia kuvipangia vyombo hivyo.
Jumla ya washiriki 250 kutoka ndani na nje ya Tanzania ikiwemo mitandao ya kijamii imealikwa kushiriki katika mkutano huo. Washiriki wengine ambao wamefanikisha WPFD-2017 ni pamoja UNESCO, TMF, UTPC, TEF, TAMWA, MCT, MOAT, Internews, UNIC na UNICEF.