Rais Magufuli Kuzinduwa Rasmi Mabasi ya Mwendo Kasi Dar

Mabasi yaendayo kasi

Mabasi yaendayo kasi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, kesho tarehe 25 /01/2017 anatarajiwa kuzindua Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji wa Huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka (Bus Rapid Transit – BRT) katika Kituo Kikuu cha Mabasi kilichopo Kariakoo eneo la Gerezani.

Uzunduzi huo utahudhuriwa na Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Bw. Makhtar Diop na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia wa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird.

 

Mabasi ya Mwendo Kasi Dar

Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yenye urefu wa kilometa 20.9 unaojumuisha barabara ya Kimara – Kivukoni, Magomeni – Morocco na Fire – Kariakoo ulikamilika Desemba 2015.

Aidha, utoaji wa huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka ulianza tarehe 10 Mei, 2016. Kwa sasa huduma ya mabasi katika kipindi cha mpito inatolewa katika njia nane, vituo vikuu vitano, vituo vidogo 28 na karakana moja kwa kutumia mabasi 140 yanayojumuisha mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja na mabasi madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.

Mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) umepangwa kutekelezwa kwa awamu sita kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

Imetolewa na:

Eng. Joseph M. Nyamhanga
KATIBU MKUU (UJENZI)
24 Januari, 2017