Na Beatrice Lyimo, MAELEZO-Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka waandishi wa habari nchini kutotumika kama mgongo kwa baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari katika kupinga muswada wa sheria wa huduma za habari wa mwaka 2016.
Aliyasema hayo leo Jijini Dar es Saalam wakati wa mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari nchini katika kuhadhimisha mwaka mmoja wa Utawala wake, ambapo alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya wamiliki wenye mashali binafsi katika kupinga mchakato mzima wa upatikanaji wa Sheria ya Huduma za Habari nchini.
“mchakato wa kupata Sheria ya huduma za habari umechelewa kutokana na sababu mbalimbali hivyo ninawataka wanahabari kutozungumza kwa mgongo wa wamiliki mbalimbali wenye maslahi binafsi katika kupinga upatikanaji wa Sheria hiyo.
Alisema kuwa suala la Muswada wa Huduma za Habari upo mikononi mwa wabunge ikiwa ni muhimili unaojitegemea na hatoweza kuingilia maamuzi ya bunge na kuacha wabunge kutimiza wajibu wao katika utungaji na upatikanaji wa Sheria hiyo.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa anafahamu baadhi ya changamoto zilizopo kwa waandishi wa habari hasa katika masuala ya maslahi hivyo muswada huo utasaidia katika kutatua changamoto hizo na pia utaifanya tasnia ya habari kuwa taaluma itakayoheshimika kama taaluma nyingine.
Akizungumza kuhusu ushirikiano baina yake na vyombo vya habari, Rais Magufuli amewataka vyombo vya habari nchini kushirikiana, kusimamia uzalendo katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo.