Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Novemba, 2016 amewaongoza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samuel John Sitta aliyefariki dunia tarehe 07 Novemba, 2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.
Mwili wa Marehemu Samuel John Sitta umeagwa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam ambapo Viongozi wengine waliojumuika kuuaga mwili huo ni pamoja na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa
Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri wakuu wastaafu Jaji Joseph Sinde Warioba na Frederick Tluway Sumaye, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Katipwa Wambali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Baada ya kuagwa katika viwanja vya Karimjee, mwili wa Marehemu Samuel John Sitta umesafirishwa kwenda Dodoma ambako Wabunge, Viongozi wa Mkoa na wananchi watapata fursa ya kuuaga katika Viwanja vya Bunge na baadaye jioni utasafirishwa kwenda Tabora ambako maziko yatafanyika kesho Jumamosi huko Urambo.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar Mhe.
Hafidh Ali Tahir kilichotokea majira ya saa 9 usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Mhe. Hafidh Ali Tahir amefariki dunia muda mfupi alipofikishwa hospitali baada ya kuugua ghafla.
“Nimeshtushwa sana na kifo cha Mhe. Hafidh Ali Tahir na ninakuomba Mhe. Spika Job Ndugai unifikishie salamu za pole kwa Familia ya Marehemu, Wabunge, Wananchi wa Jimbo la Dimani, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huu.
“Tutamkumbuka Mhe. Hafidh Ali Tahir kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika utumishi wa umma, katika michezo na akiwa mwakilishi wa wananchi, kwa hakika tumepoteza mtu muhimu sana” amesema Rais Magufuli na kumuombea Marehemu apumzishwe mahali pema peponi. Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Novemba, 2016
Rais Mstaafu wa awamu awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiaga mwili wa Marehemu Samwel John Sitta Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Novemba 11,2016
Rais Mstaafu wa awamu awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Wiliam Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa wakiaga mwili wa Marehemu Samwel John Sitta Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Novemba 11,2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt . John Pombe Magufuli akimfariji Mama Margareth Sitta, Mjane wa aliyekuwa Spika Mstaafu Marehemu Samwel John Sitta alipoongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa kiongozi huyo mkongwe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam Oktoba 11, 2016