RAIS wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufulia na Makamu wake, Mama Samia Suluhu wamevunja ukimya jana jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa kasi ya utendaji wa Serikali yake si nguvu za soda kama wanavyokejeli baadhi ya watu. Rais Magufuli alisema wanaodhani kasi yake na watendaji wake ni nguvu za soda watasubiri sana huku wao wakiendelea kutumbua majipu moja baada ya lingine.
Kiongozi huyo wa nchi ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wazee wa jiji la Dar es Salaam katika maadhimisho ya Serikali yake kutimiza siku 100 tangu waingie madarakani.
“…Mimi na serikali yangu tumejitoa sadaka kwa ajili ya watanzania, tunaomba muendelee kutupa nguvu ili haya matamanio yetu kwa ajili ya Tanzania yoyote tena kwa hara. Yoyote atakaejaribu kutukwamisha serikalini tutambomoa kwa ajili ya watanzania,” alisema Rais Magufuli.
“…Zipo kejeli nyingi kuwa ni nguvu ya soda, hata kama ni soda ukiweka gongo utalewa, kwa hio hii ni soda special. Tumeweka bilioni 200 kwa ajili ya daraja la Coco Beach hadi Agha Khan, barabara ya kutoka Rangi tatu pia tumeitengea fedha na interchange ya ghorofa tatu pale Ubunge,” alisema Rais.
Napenda niwahakikishie wazee na watanzania kwa ujumla, hatutawaangusha. Kwa niaba ya viongozi wenzangu, nawaahidi tutawanyia kazi, ninachowaomba wazee na watanzania kwa ujumla, mtuamini. Katika shughuli zozote za kufanya mabadiliko huwa kuna changamoto zake, watakaoguswa ni wachache sana kwa ajili ya watanzania wote hasa maskini. Haipaswi kuwa maskini, Tanzania hii ina utajiri wa kila aina, haipaswi kuwa na wanafunzi wanaokaa chini, watu wanaolala chini mahospitalini.
Lakini ni lazima tujue wapo watu wachache waliotufikisha hapa, mlituchagua kwa mioyo yenu wote, ndio maana nasema kwa dhati naomba mtuamini kwa sababu tunaamini tukiyatekeleza haya, nchi hii itakuwa ya mfano Afrika kama si duniani kwa ujumla.
Wapo watu kwao pesa si tatizo na angalau wangezipata kihalali, lakini ni za wananchi wenye hali mbaya sana Kilometa moja imejengwa kwa bilioni mbili tena ni barabara ya halmashauri, nimekaa serikalini miaka 20 na sijawahi kutengeneza barabara kuu, kilometa moja kwa bilioni mbili lakini barabara ya halmashauri tena ya Bariadi inatengenezwa kwa mabilioni ya shilingi zilizokuwa zinatoisha kutengeneza zaidi ya kilomita 20.
Waziri alienda kuangalia mafuta, PUMA na ORLX serikali ina share ya asilimia 50. Flow meter ambayo ndio inapima mafuta kiasi gani yanaingia nchini hakifanyi kazi miaka mitano na Dar es Salaam kila kona sheli. Nilikutana na wakina mama wakaniambia twende ukaone, nilishaenda lakini ilikuwa upande mwingine, wasaidizi wangu wakaniambia usiende lakini nikaenda. Nikakuta maji ya kutoka chooni yanaingia, wakina mama wamelala chini wakati kuna jengo linajengwa tangu awamu ya mzee Mwinyi halijaisha mpaka leo.
Wazee tunapochukua hatua, sisi si wakatili sana, tunawawakisha nyinyi uchungu wenu. Ninafahamu mawaziri wangu wanafanya kazi nzuri. Ninawapa muda na nyinyi muwape muda na mimi mnipe muda. Lile jengo linalotumika kama ofisi ya uzazi wa mpango wahame na waziri atajua atawapeleka wapi tena ofisi kama ya waziri, anaweza kwenda kukaa nao ofosini kwake, wale kina mama waliokuwa wanalala chini wahamie hapo.
Ninawaomba katika kipindi hiki cha mpito mtuvumilie, majipu tutayambua kweli kweli. Tanzania haiwezi kwenda mbele bila kuwa na fedha zake, wafanyabiashara wanakwepa sana kodi. Tunataka fedha tunazozikusanya ziende kuwasaidia watanzania wa hali ya chini.
Shirika la ndege tunataka kulifufua ndio maana tunachukua hatua mbalimbali. Yuko mmoja ameshikwa pale alikuwa anataka kubadilisha fedha kwenye akaunti tukamkamata, hatutaki kusema mengi kwa sababu hatua zinachukuliwa ikiwemo za kimahakama.
Watanzania tujifunze kulipa kodi, chochote unachoenda kununua omba risiti. Kuna sehemu inatakiwa kubaki kwa ajili ya kuhudumia watu. Nimemuona Makonda akihamasisha, limekujengea heshima kubwa kwa hio ukipanda hata cheo, watu wasikuonee kwa sababu you deserve it.
Kwa sababu na sisi tunakaa Dar, nilikuwa nazungumza na makamu na waziri mkuu. Tunaokaa Dar ikiwemo mawaziri na makatibu wakuu, nikasema kwa sababu wakati nafanya uteuzi na hawakuniomba, nikiwaambia leo watoe milioni moja moja ni vibaya? Tunakusanya milioni 80 bado kuna mimi, kisha tutatenga bilioni mbili tuzigawe hizo fedha Dar ili zikajengwe hizo shule.
Michango ni hiari, pasitokee watu kupitia hii hotuba wakaanza kulazimisha watu, watakaoguswa kuchangia wachangie. Najua sijateua wakuu wa mikoa, ma-DC na wakurugenzi, nimefanya makusudi ili niendelee kuchangia nani anatosha na nani hatoshi, kutosha kwao ni kutatua kero za wananchi. Yapo magazeti mengine wanaandika mpaka unashangaa, unajiuliza yakitokea machafuko wana mahali pa kwenda kukaa. Nayapongeza magazeti mengi mfano gazeti la Jamhuri lilivoenda kufufua uozo wa Flow meter.
Akizungumzia suala la Zanzibar alisema; “…kama tume za uchaguzi nyingi duniani, haiwezi kuingiliwa na Rais yeyote ndiyo maana tume za uchaguzi huwa huru. Napenda kuheshimu sheria lwa hio ZEC ina uhuru wa kuamua mambo yake lakini kama kuna tafsiri mbaya, waende mahakamani, mahakama ziko pale halafu unamwambia Magufuli ingilia.
Jukumu langu kama amiri jeshi mkuu ni kuhakikisha amani ya Zanzibar inaimarika, yeyote atakaeleta fyoko fyko ajue vyombo vya usalama vipo. Kwa niaba ya serikali ninayoiongoza, sisi tuko makini, niwahakikishie tutaweza na Tanzania tutaivusha, itaenda mbele kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wote. Naomba wazee wangu na watanzania kwa ujumla mtuombee, wanaolalamika wachache muwapuuze kwa sababu ni miongoni ya waliofaidi matunda ya wanyonge kwa miaka ya nyuma,” alisema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais, Samia Suluhu alisema; “Tunazungumzia leo mafanikio ya siku 100 katika ofisi, naomba niwaahidi, mwendo huu utakuwa ni wa kudumu, waliosema tuna nguvu ya soda naomba watuangalie. Hatutawaangusha, tuko pamoja nanyi, Tanzania Oyee, Nawashukuru sana.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick akiwasalimu wazee anasema; “Baada ya kutangaza elimu bure, wanafunzi waliofikia umri wa kuanza shule na waliopitiliza wamekuwa wakiandikishwa kwa wingi. Kwa utaratibu wa wizara ya elimu uandikishaji unaendelea 31/3/2016, shule zimendikisha wanafunzi wengi kuliko malengo mfano Mzinga walilenga kuandikisha 100 lakini mpaka juzi walishaandikisha wanafunzi 541.
Niishukuru kampuni ya TSN kwa kukubali kujenga darasa moja katika shule ya majimatitu pia tuliiga mfano wako wa kubana matumizi na tulikutana kuangalia maeneo gani tuliyoyatengea fedha ili kuweza kubana ikiwemo safari na tumeweza kuokoa bilioni 4.6 na wewe tulikuomba kuhamisha hizi tija kuelekea maeneo yenye tija na umeshaturuhusu kutumia hizo pesa kwenye mambo ya maendeleo, tunakushukuru sana.
Tunahamasisha wakazi wa Dar kuhamasika kuchangia elimu kwa hiari ikiwemo madawati na hapa hatupingani na sera ya elimu bure na wapo wenzetu wameshaonyesha nia ikiwemo Azim Dewji madawati 500, ubalazi wa China ambayo tumeyapeleka Majimatitu na wengine wengi. Nichomekee tu, hata meza kuu wanaweza kuchangia kwa ajili ya maendeleo ya Dar es Saalaam. Katika kuchangia kutatua changamoto za elimu, wanasiasa pia nawaomba washiriki bila kujali chama, sote tunajenga nyumba moja haina haja kugombania fito.