Rais Magufuli ‘Avamia’ Wizara ya Maliasili na Utalii…!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipunga mkono kuagana na mgeni wake Mfalme wa Morocco Mohamed VI aliyemaliza ziara yake ya kikazi na kuondoka jijini Dar es Salaam Oktoba 27,2016 (Bofya blog kwa habari na picha)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipunga mkono kuagana na mgeni wake Mfalme wa Morocco Mohamed VI aliyemaliza ziara yake ya kikazi na kuondoka jijini Dar es Salaam Oktoba 27,2016 (Picha na Ikulu)

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 29 Oktoba, 2016 amefanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House) kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili inayofanywa na Kikosi Kazi kilichoundwa na Wizara hiyo.

Akiwa katika ofisi hizo Rais Magufuli aliyekuwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudensi Milanzi ameshuhudia pembe 50 za ndovu zilizokamatwa kati ya jana Ijumaa na leo Jumamosi Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Magufuli ameoneshwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamebeba pembe hizo na watuhumiwa wanane wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya pembe za ndovu.

Rais Magufuli amewapongeza askari wote waliopo katika Kikosi Kazi cha kudhibiti na kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu pamoja na Raia wema wote wanaotoa ushirikiano katika operesheni hiyo na amewahakikishia kuwa anatambua kazi kubwa wanayoifanya na anawaunga mkono.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na ninawahakikishia kuwa ninawaunga mkono, chapeni kazi, wakamateni wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa au nani, kamateni, wala msijali cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno, watafuteni wote mpaka watu wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe ili tuokoe wanyama wetu ambao wanaendelea kutekelezwa.

“Hapa mmekamata pembe 50 maana yake tembo 25 wameuwawa, haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwa sababu ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka” amesisitiza Rais Magufuli.