RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo asubuhi tarehe 25 Septemba, 2016 ameungana na Waumini wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano lililopo Posta Jijini Dar es Salaam kusali ibada ya Jumapili ya kuadhimisha Siku ya Bwana ya 19 baada ya Pentekoste.
Akizungumza na Waumini wa Kanisa hilo baada ya kumalizika kwa Ibada, Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru Viongozi na Waumini wa Kanisa la Anglikana na Madhehebu mengine ya Dini hapa nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani na utulivu.
Dkt. Magufuli amesisitiza kuwa Viongozi wa Dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na Viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.
“Ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuliombea Taifa hili, ninawashukuru kwa sababu siku zote mmekuwa mkipiga magoti na kumtanguliza Mungu mbele, ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuombea amani ya nchi yetu na upendo udumu ndani yetu sisi sote.
“Makanisa yote, Madhehebu yote, Dini zote, Vyama vyote, upendo tukiujenga ndio tutaiendeleza vizuri Tanzania yetu” Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Padre Jackson Sostenes aliyeongoza Ibada hiyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa Kanisa hilo katika Ibada ya Jumapili na ameahidi kuwa Viongozi na Waumini wa Kanisa hilo wataendelea kumuombea na kuliombea Taifa.
Katika Ibada hiyo Rais Magufuli ametoa Shilingi Milioni 1 kuchangia vikundi vya kwaya vya kanisa hilo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Septemba, 2016