RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samuel Sitta.
Mhe. Samuel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samuel Sitta na kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samuel John Sitta, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichotokea usiku wa jana tarehe 6/11/2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alipokuwa akitibiwa.
Taarifa ya CCM iliyotolewa na Msemaji wake, Christopher Ole Sendeka; imeeleza Mhe. Samuel John Sitta, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi katika Chama na Serikali. Alikuwa Katibu wa CCM na Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha uwekezaji, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge, Waziri na Spika.
Mhe. Sitta alikuwa ni Kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliyejitambulisha kwa utendaji wenye kufuata falsafa yake ya “kasi na viwango”. Ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Chama na Serikali.
Katibu Mkuu wa CCM Ndg Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, familia ya Mhe. Sitta pamoja na Wananchi wa Jimbo la Urambo kufuatia kifo cha Kiongozi huyu. Tunaungana nao katika msiba huu ambao pia ni msiba wetu. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Ameni