Rais Magufuli Alilia Suluhu Nchi ya Sudan Kusini…!

Mwenyekiti wa EAC na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Mwenyekiti wa EAC na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Na Ismail Ngayonga, MAELEZO-Dar es Salaam

RAIS John Pombe Magufuli amewataka Viongozi na wananchi wa Sudan Kusini kutanguliza mbele maslahi ya nchi yao ili kusaidia kumaliza mgogoro wa kisiasa unaondelea nchini humo.

Akizungumza katika mkutano wa 17 wa Jumuiya hiyo leo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli alisema jumuiya hiyo inasikitishwa na mapigano ya ghafla yaliyoibuka hivi karibuni nchini humo.

Rais Magufuli alisema suala la amani na usalama ni jambo umuhimu si kwa ustawi wa maendeleo ya taifa hilo pekee bali pia kwa mustakabali wa mataifa mengine yaliyopo ndani ya jumuiya hiyo.

Aidha Rais Magufuli aliipongeza Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika (IGAD) inayoundwa na nchi za Eritrea, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda katika jitihada zake kusuruhisha mgogoro huo.

Aidha Rais aliipongeza nchi ya Sudan Kusini kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya hiyo na kuwahakikishia kuwa jumuiya hiyo itatoa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha ikuwa nchi inapata amani ya kudumu ili wananchi wake washiriki katika shughuli za maendeleo.

“Sekretarieti ya jumuiya hiyo inaendelea na maandalizi ya kujumuisha nchi ya Sudan Kusini katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na nchi wanachama” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, mwakilishi maalum wa Rais wa Sudan Kusini, Aggrey Tisa Sabuni aliishukuru jumuiya hiyo kwa uamuzi wa kuikubali nchi hiyo kuwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo na kuwakikishia kuwa taifa hilo litarejeshea hali ya utulivu na usalama.

“Jaribio la mapinduzi la mwezi julai mwaka huu limeleta athari kubwa kwa wananchi wetu, hata hivyo tunawahakikishia kuwa tutakuwa mshirika wa kweli wa jumuiya hii” alisema Sabuni.