Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
SERIKALI imeikabidhi Mahakama ya Tanzania kiasi cha Sh. bilioni 12.3 zilizoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria kwa lengo la kuiwezesha Mahakama kuimarisha utendaji kazi na kutekeleza majukumu yake inapasavyo.
Akikabidhi fedha hizo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema kuwa fedha zilizokabidhiwa kwa Mahakama ni mwitikio wa kutekeleza ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Duniani Januari 4, 2016.
“Ni matumaini ya Serikali fedha hizo zitatumika vizuri na zitatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa,” alisema Dk. Mpango.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju amemshukuru, Rais kwa kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ndani ya siku nne na kuudhihirishia umma kuwa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” anaisimamia kwa vitendo.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mhakama, Hussein Katanga alisema kuwa fedha walizokabidhiwa zitasaidia ujenzi wa mahakama nchini na zipo ndani ya bajeti ya mwaka 2015/2016 na watazitumia kulingana na malengo yaliyokusudiwa.