RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 15 Mei, 2017 ameivunja rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na ameagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli ameivunja CDA kwa kutia saini hati ya Amri ya Rais ya kuivunja Mamlaka hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam, tukio ambalo limeshuhudiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Antony Mavunde, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana na viongozi mbalimbali wa wizara.
Mhe. Rais Magufuli amesema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA.
Kufuatia uamuzi wa kuivunja CDA, Mhe. Dkt. Magufuli pia ameivunja Bodi ya CDA, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA Mhandisi Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine na ameagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadiri inavyofaa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33 zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini ili kuwavutia wawekezaji hasa wa viwanda.
“Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sana, hata nilipokuwa kwenye kampeni zangu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walilalamika sana, sasa nimetekeleza niliyowaahidi, naamini kwa uamuzi huu malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia tutakuwa tumeondoa kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma.
“Sasa majukumu yote yanahamishiwa Manispaa ya Dodoma, sitaki kuendelea kusikia visingizio, mkajipange mambo yaende vizuri” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi huo na wameahidi kusimamia kwa ukaribu mchakato wa kuhamisha majukumu ya CDA kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ilianzishwa kwa Amri ya Rais ya tarehe 01 Aprili, 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230 na imevunjwa rasmi leo tarehe 15 Mei, 2017 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa katika gazeti la Serikali.