Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete yuko mjini Windhoek, Namibia kwa ziara ya kikazi ya siku moja nchini humo. Rais Kikwete ameondoka nchini asubuhi ya Agosti 11, 2011, na atarejea baada ya ziara hiyo.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) yuko Namibia kuhudhuria mkutano wa wakuu wa vyama vya siasa vilivyopigania uhuru miongoni mwa nchi za kusini mwa Afrika.
Katika mkutano huo wa leo, chama tawala cha Nambia cha SWAPO kinavikaribisha vyama vya CCM, ANC cha Afrika Kusini, Frelimo cha Mozambique, MPLA cha Angola na ZANU-PF cha Zimbabwe.
Mkutano huo wa siku moja unalenga kuangalia historia ya uhusiano baina ya vyama hivyo, na jinsi historia hiyo inavyoweza kutumika kuongeza ushirikiano baina ya vyama hivyo katika mazingira ya sasa.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo muhimu miongoni mwa vyama ambavyo viliongoza mapambano ya kisiasa, na kwenye nchi nyingi pia mapambano ya kijeshi na vita ya ukombozi, ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilsom Mukama.