RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Februari 27, 2014, ameungana na mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Fulgence Kazaura katika shughuli ya heshima za kuaga mwili iliyofanyika Ukumbi wa Nkrumah, Chuoni hapo.
Rais Kikwete aliwasili kwenye ukumbi huo kujiunga na Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waliokuwa Mawaziri Wakuu, Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Makamu wa Chuo Kikuu hicho Profesa Rwekaza Mukandala, familia ya marehemu na waombolezaji wengine muda mchache klabla ya kuanza shughuli ya kuaga mwili.
Marehemu Kazaura ambaye alikuwa Mkuu wa UDSM kati ya mwaka 2005 hadi kifo chake, aliaga dunia Jumamosi iliyopita katika Kituo cha Ugonjwa wa Kansa mjini Chennai, India na mwili wake uliwasili nchini Jumanne wiki hii. Mazishi ya marehemu yamepangwa kufanyika keshokutwa Jumamosi, Machi Mosi, 2014, nyumbani kwao Bukoba.
Katika uhai wake alishikilia nafasi nyingi za utumishi ikiwa ni pamoja na kuwa RDD, Katibu Mkuu wa Wizara mbali mbali, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya na Ubelgiji, na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashariki.