Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa walimu wa Tanzania wanao uwezo wa kufundisha somo la Kiingereza vizuri kama wakiwezeshwa kwa kupatiwa vitabu vya kiada vilivyojaribiwa, tahiniwa na kupimwa (tried and tested text books) kwa ubora wake kama moja ya njia muhimu za kuinua kiwango cha elimu nchini.
Aidha, Rais Kikwete amewataka wadau wa elimu kushirikiana katika kubaini vitabu hivyo ambavyo amesema kuwa kwa miaka mingi vimethibitika kuwa bora zaidi katika kuwafundishia watoto na wanafunzi wa Tanzania. Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumatatu, Novemba 14, 2011, Ikulu, Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Bibi Katy Allen, mtunzi wa vitabu vya lugha ya Kiingereza vya Oxford.
Bibi Katy Allen alikuwa anamwelezea Rais Kikwete kuhusu jitihada ambazo shirika lake lisilokuwa la kiserikali la Village Education Project Kilimanjaro (VEPK) limekuwa linafanya kuchapisha na kuboresha kutunga vitabu vya kufundishia na kujifunza lugha ya Kiingereza vya Oxford Engilish Books vilivyokuwa vinatumika kufundishia lugha hiyo nchini katika miaka ya nyuma.
Bibi Katy Allen anasema kuwa shirika lake linaamini kuwa kama vitabu hivyo vikianza kutumika tena katika shule za Tanzania, ufundishaji wa lugha ya Kiingereza unaweza kuboreka haraka zaidi. Vitabu hivyo vilivyokuwa vinatumika kuanzia shule za msingi hadi shule za kati, yaani kuanzia darasa la tatu hadi la nane, viliacha kutumika kwenye miaka ya 1970 baada ya kufanyika mageuzi katika mfumo wa elimu nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Bibi Katy Allen wamejadili kwa undani kuhusu ufundishaji wa somo la lugha ya Kiingereza na jinsi gani ufundishaji wa lugha hiyo unaweza kuboreshwa kwa kutumia vitabu hivyo ambavyo mama huyo ameviandika upya kwa kusaidiwa na mwomgoza wa mwalimu.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amesema kuwa ni dhahiri walimu wa Tanzania wanaweza kufanya kazi nzuri zaidi kama watawezeshwa na wadau mbalimbali wa elimu kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kupatiwa vitabu bora zaidi vya kiada vya kuongoza namna bora zaidi ya mbinu za ufundishaji.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Michio Ogimura, Makamu wa Rais Mtendaji na Mshauri Maalum wa Kampuni ya Sumitomo ya Japan katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemwelezea kiongozi huyo kuhusu fursa za uwekezaji zilizoko Tanzania hasa katika eneo la nishati na madini.