Na Mwandishi Maalumu, Perth, Australia
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema changamoto kubwa ya sasa ya uwekezaji katika Afrika ni kwamba uwekezaji huo lazima ulenge na ufanikishe kuwanufaisha Waafrika walio wengi na siyo kuwanufaisha wawekezaji wageni tu.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa uwekezaji katika Afrika uwe ni uwekezaji ambao unaongeza thamani kwenye maisha ya watu kwa kupunguza na hatimaye kukomesha umasikini, kwa kuongeza uwezo wa watu kupata chakula cha uhakika zaidi na kupata ajira za uhakika zaidi.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Biashara katika Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola (Commonwealth Business Forum), Dk. Mohan Kaul kwenye Hoteli ya Hyatt Regency mjini Perth, Australia, ambako Rais Kikwete amefikia. Wote wawili wako Perth, Australia kuhudhuria Mkutano wa Nchi za Jumuia ya Madola (CHOGM).
Dk. Kaul alikuwa anazungumza na Rais Kikwete kuhusu ratiba ya shughuli za kesho ambako Rais Kikwete atazungumza kwenye mkutano wa Commonwealth Business Forum ikiwa sehemu ya ratiba yake kwa ajili ya CHOGM.
Rais Kikwete amemwambia Dk. Kaul kuwa ni muhimu kwa Jumuia ya Madola kuelekeza nguvu sawa katika kuzisaidia nchi masikini wanachama wake kuondokana na umasikini kwa nguvu na kasi ili ile ya Jumuia hiyo kutaka kuimarisha masuala ya ujenzi wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
“Changamoto kubwa kwa Jumuia yetu sasa ni jinsi ya kuzisaidia nchi masikini za Afrika kuondokana na umasikini na jinsi gani ya kusaidia mataifa madogo ya Jumuia hiyo ambayo pia ni visiwa (small island states) kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni jambo zuri kuwa katika Jumuia ya Madola tumeelekeza nguvu za kutosha katika masuala ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu. Hili ni jambo zuri. Sasa ni wakati pia kwa nchi tajiri ndani ya Jumuia yetu kusaidia nchi masikini katika kuwekeza zaidi, katika kuinua biashara yao ili kuziwezesha nchi hizo kuondokana na umasikini.”
Rais Kikwete amesema kuwa changamoto kubwa za Jumuia hiyo mbali na mambo mengine ni jinsi ya kuzisaidia na kuziwezesha nchi masikini ambazo ndiyo nyingi zaidi miongoni mwa wanachama wa Jumuia ya Madola kuondokana na umasikini, kupunguza ukosefu wa ajira na kutafuta njia za kugawana vizuri utajiri utakaopatikana kutokana na juhudi hizo.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Shell, Guy Outen. Katika mkutano huo, viongozi hao wawili wamezungumzia mipango ya kampuni hiyo katika kuwekeza katika utafutaji wa gesi asilimia katika bahari ya Hindi.