RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete amelaani kwa mara nyingine vitendo “vya aibu” vya mauaji ya albino kwa sababu za kishirikina, akiapa kuwa Serikali itahakikisha kuwa aibu hiyo inakomeshwa kabisa nchini.
Rais Kikwete pia amefafanua kuwa tatizo la mauaji ya albino katika Tanzania siyo tatizo la haki za binadamu wala tatizo la ubaguzi, bali ni tatizo la ushirikina ambao umevuka mipaka.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni hatua kali za Serikali ambazo zimefanya mauaji ya albino kwa sababu za ushirikina kupungua kwa kiasi kikubwa hata kama halijamalizika kabisa.
Rais Kikwete amelaani vitendo hivyo vya mauaji ya albino wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki Moon ambaye alitaka kujua maendeleo yaliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na mauaji ya albino.
Rais Kikwete amemwambia Ban Ki Moon: “Ni kweli tumekuwa na tatizo la mauji ya albino. Lakini tatizo hili siyo tatizo la haki za binadamu ama tatizo la ubaguzi. Tatizo la mauaji ya albino ni tatizo la ushirikina wa aibu kubwa kwa nchi yetu na aibu sana kwa jamii yetu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Baadhi ya watu wetu bado wanaamini kuwa kukata mkono ama kidole cha albino kunaweza kusaidia maendeleo ya biashara kama kwenye uvuvi, kwa mfano. Ni aibu kubwa kwa taifa letu.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesisitiza kuwa mauaji ya albino katika Tanzania yamepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka miwili, mitatu iliyopita hata kama hayajaisha kabisa kwa sababu ya hatua kali ambazo zimechukuliwa na Serikali.
“Kwa hakika, Serikali imechukua hatua kali katika miaka miwili, mitatu iliyopita ikiwa ni pamoja na kupiga kura ya maoni kuwasaka wauaji wa albino ambao sasa wamefikishwa mahakamani na baadhi yao wamehukumiwa kifo. Tumefika hapa kwa sababu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali na tutaendelea kukabiliana na tatizo hili mpaka liishe kabisa,” Rais amemwambia Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Wakati huo huo, Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Mtawala wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mheshimiwa Helen Clark ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu wa New Zealand.