*Asema vigogo wengi tayari wako kizimbani
Na Hassan Abbas, Addis Ababa
RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi huku pia akikemea chokochoko za kidini alizosema ni kiashiria kikubwa cha kuvunjika kwa amani ya Tanzania iliyodumu kwa miaka 50 sasa.
Rais Kikwete aliyasema hayo mjini hapo wakati akitoa maelezo yake mara baada ya kuwasilishwa ripoti ya Hali ya Utawala Bora Tanzania kwenye kika cha Viongozi wa Nchi za Umoja wa Afrika Zinazhoshiriki katika Mpango wa kujitathmini Kiutawala Bora (APRM)
Akisoma Ripoti ya Utawala Bora Tanzania, Kiongozi wa Jopo la Wataalamu wa APRM, Barrister Akere Muna alisema katika eneo la rushwa Tanzania kama nchi nyingine za Afrika imekumbwa na tatizo hilo hasa katika eneo la manunuzi ya umma.
Katika Ripoti yake, Barrister Muna aliyeongoza jopo la wataalamu 21 kuja Tanzania Machi, 2011 kufanya uhakiki wa Ripoti hiyo kwa kukutana na wananchi na viongozi mbalimbali, pia alisema Ripoti yao imebaini juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kupambana na ufisadi ikiwemo kuwaondoa mawaziri waliotuhumiwa na kuwashitaki maofisa wengine wandamizi.
Rais Kikwete akijibu kuhusu suala la rushwa alisema Serikali ya Tanzania imekuwa ikayachukulia kwa umakini na ukali mapambano dhidi ya rushwa tangu ulipopatikana uhuru wa iliyokuwa Tanganyika mwaka 1961.
“Enzi za Mwalimu tulianza kwa ukali dhidi ya rushwa. Wakati ule tuliweka adhabu ya kifungo lakini na viboko. Nakumbuka Mwalimu Nyerere alikuwa akisema tunakuchapa viboko 12 utakapoingia gerezani na 12 siku unayotoka,” alisema Rais Kikwete.
Katika mkutano huo ambapo nchi za Tanzania na Zambia ziliwasilisha Ripoti zao, Rais alisema wakati wa utawake alianza kwa kuimarisha taasisi za kupambana na rushwa na kuendeleza sera ya uwazi katika mapambano hayo.
“Nashukuru kuona ripoti ya utafiti ya APRM imebaini changamoto ya rushwa inayoikabili nchi yetu na nchi nyingine za Afrika. Nashukuru pia kwa Ripoti kutambua jitihada kubwa tulizoanza kuzichukua katika kupambana na rushwa.
“Serikali yangu itaendelea kutovumilia vitendo vyovyote vya rushwa na ufisadi. Leo hii ninavyozungumza wapo mawaziri na viongozi wengine waandamizi wakiwemo mabalozi walioshawahi kufikishwa mahakamani,” alisema.
Aliwaambia viongozi wenzake wa Afrika kuwa ukali wake dhidi ya rushwa umewakumba hata watu ambao wengine ni marafiki zake wa karibu. “Miongozi mwa waliofikishwa kortini baadhi ni marafiki zangu kabisa niliokuwa nao kwenye Baraza la Mawaziri wakati nami nikiwa Waziri na maofisa wengine walikuwa chini ya Serikali yangu ya sasa nikiwa Raisi,” alisema Rais Kikwete.
Vurugu za kidini
Ripoti ya Barrister Akere Muna ilieleza kuwa moja ya misingi mikuu ya maendeleo nchini Tanzania ni hali ya amani na mshikamano iliyodumu kwa miaka 50 ya uhuru. Hata hivyo Ripoti hiyo iliishauri Serikali ya Tanzania kufanyiakazi changamoto zinazojitokeza.
Akijibu suala hilo, Rais Kikwete alikiri kuwa moja ya changamoto zinazoikabili Serikali yake na kiasshiria anachoona kinaweza kuharibu amani ya Tanzania ni chokochoko za kidini.
“Hili ni eneo ambalo lazima nikiri linatupa changamoto kubwa. Kama inavyofahamika kuwa nSerikali yetu si ya kidini lakini imewapa uhuru watu wake kuabudu na kuzitangaza dini zao. Serikali ya Tanzania inaona hapa kuna mambo ya kufanywa kukabiliana na baadhi ya watu wanaotaka kutumia dini kuvuruga amani.
“Suala hili linanipa shida sana. Wakati mwingine unafikiria labda watu wamechoka amani wanataka kuona vita ikoje. Msimamo wa serikali yangu ni kwamba hatutavumilia tena vitendo hivyo na hatutasikiliza kelele za watu, tutaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanasiasa au viongozi wa dini watakaochochea vurugu hizo,” alisema.
Rais alitumia fursa hiyo kuwashauri viongozi wa dini mbalimbali nchini Tanzania kuendeleza ushirikiana kwa kukutana katika majukwaa yao na kukemea viashiria vyovyote vinavyoweza kuleta chokochoko za kidini.
Ripoti ya Tanzania imesifiwa na viongozi wengi wa Afrika kuwa ni ya mfano wa nchi inayoweza kuwa fundisho kwa nchi nyingine nyingi Barani Afrika. Marais kadhaa wameahidi kuja Tanzania kujifunza zaidi kuhusu masuala mbalimbali.
Mbali ya Rais Kikwete mkutano huo pia ulihudhuriwa na Marais wa nchi za Afrika Kusini, Rwanda, Benin, Zambia, Senegali, Chad, Tunisia, Waziri Mkuu wa Ethiopia huku nchini nyingine zikiwakilishwa ama na Mawaziri Wakuu au mawaziri waandamizi.