Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa siasa ya nchi za nje na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano ya Tanzania na nchi za kigeni hayatabadilika hata baada ya yeye kuondoka madarakani mwanzoni mwa Novemba, mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuwa yeye anaondoka madarakani lakini Tanzania waliyoizoea na kuijua itabakia pale pale na kuwaomba viongozi hao kumpa ushirikiano mkubwa mrithi wake kama walimpa yeye.
Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo mara mbili leo, Jumapili, Juni 14, 2015, wakati alipohutubia kuwaaga wakuu wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wakati wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika uliofunguliwa leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Sandton Convention mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Wakati wa mkutano ujao wa kawaida wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, Januari, mwakani, Tanzania itakuwa na Rais mpya, Rais wa Tano.
Aidha, Rais Kikwete amerudia kauli na msimamo huo wa Tanzania wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Somalia, Mheshimiwa Hassan Sheikh Mahmoud ambako kiongozi huyo wa Somalia amemjulisha Rais Kikwete kuwa angependa kutembelea Tanzania baadaye mwaka huu.
Alisema Rais Kikwete kuwa misingi ya siasa za nchi za nje za Tanzania na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano yake na nchi za nje yaliwekwa tokea Uhuru na hasa tangu kutungwa wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania mwaka 1972 na tokea wakati huo hajapata kubadilika kama kama wamebadilika viongozi mara nne sasa.
“Hatujapata kubadilisha misingi hiyo inayoelekeza kuwa mahusiano yatajengwa kuanzia nchi za jirani, zikifuatiwa na nchi za Afrika, nchi marafiki duniani na nchi nyinginezo.”
“Sina shaka kabisa kuwa misingi ya siasa za nje na misingi mikuu ya uongozi wan chi yetu itabakia ile ile isipokuwa kama Rais ajaye atatoka chama kingine. Kitakachobadilika ni staili ya uongozi tu lakini misingi ya uongozi itabadilia pale pale kwa sababu ni misingi mizuri, ni misingi ya busara ambayo imeongoza nchi yetu vizuri kwa miaka mingi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Ni matumaini yangu kuwa Watanzania tutachagua kiongozi mzuri atakayeendela kutoa kipaumbele cha juu kwa masuala ya Afrika pamoja na uanachama na ushiriki wetu katika Umoja wa Afrika. Haya ni miongoni mwa misingi mikuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania tangu uhuru mpaka sasa. Nawaomba mumpe ushirikiano mkubwa kama mliopnipatia mimi na hata kuzidi.”