Rais Kikwete, Rais Rajoelina Wazungumza kwa Kina Mgogoro wa Madagascar

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina (kulia).

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina Julai 22, 2013 wamekutana kwa mazungumzo ya muda mrefu kuhusu mgogoro wa kisiasa katika Madagascar na njia za kuweza kutoka katika mgogoro huo.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam yaliendelea kwa zaidi ya dakika 75 na Rajoelina alimweleza Rais Kikwete kuhusu hali ya kisiasa ilivyo katika Madagascar na kuomba ushauri kutoka kwa Kikwete kuhusu jinsi gani ya kukabiliana na hali hiyo.

Rais Rajoelina amemwambia Rais Kikwete mwanzoni mwa mazungumzo hayo: “Mheshimiwa Rais, nianze kwa kukushukuru kwa dhati ya moyo wangu kwa kuwa binadamu ambaye umetusikiliza sana. Tunakushukuru sana kwa juhudi zako na ari yako binafsi kujaribu kufanikisha zoezi la kuitoa Madagascar katika kipindi inachopitia. Ni wakati wa shida, kama huu kwetu, unapopata kujua marafiki wa kwelikweli. Kwahakika, Rais, umekuwa rafiki halisi wa nchi yetu.”

Rais Kikwete naye alitumia muda kumweleza Rajoelina jinsi Tanzania, nchi nyingine na taasisi nyingine muhimu za kisiasa duniani, ikiwamo Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuia ya Ulaya(EU) zinavyoina hali ya Madagascar na njia zipi zinaweza kutumika kukitoa Kisiwa hicho kikubwa kuliko vyote katika Afrika katika mgogoro wa sasa.

Viongozi hao wawili wamekubaliana kukutana tena asubuhi ya Julai 23, 2013, kuendelea na mazungumzo kwa nia ya kupata majawabu ya kwelikweli na yanayoweza kukubalika kwa pande zote zinazovutana katika Madagascar kuhusu jinsi gani ya kuitoa nchi hiyo katika matatizo yake ya sasa.

Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Troika-Organ) ya SADC ndiye amepewa jukumu na viongozi wenzake wa SADC kutafuta majawabu katika migogoro ya kisiasa inayozikabili nchi wanachama wa SADC ikiwamo Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Zimbabwe.

Kikwete amekuwa anahangaika na mzozo wa Madagascar na mara tatu amemwalika Rais Rajoelina kuja nchini kwa mazungumzo yenye lengo la kumaliza mgogoro katika nchi hiyo. Mapema jana mchana, Rais Kikwete amempokea Rais Rajoelina na ujumbe wake kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa mazungumzo ya baadaye jioni.