Rais Kikwete mgeni rasmi Mkutano Mkuu wa Holy Ghost Missionaries

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amealikwa kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano Mkuu (General Chapter) wa 20 wa Shirika la Ukasisi wa Holy Ghost Missionaries la Kanisa Katoliki duniani utakaofanyika mjini Bagamoyo kuanzia Juni 24, mwaka huu, 2012.

Rais Kikwete amekabidhiwa mwaliko huo na Askofu wa Jimbo la Morogoro, Baba Askofu Telesphor Mkude wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, Februari 14, 2012, Ikulu, Dar es Salaam.

Tayari Rais Kikwete amekubali mwaliko huo wa Jimbo la Tanzania la Holy Ghost Missionaries kushiriki katika mkutano huo utaojumuisha wajumbe 115 kutoka pote duniani kwenye hosteli ya Stella Maries kwenye mji wa Bagamoyo, mahali lilipozaliwa Kanisa Katoliki katika Afrika Mashariki mwaka 1868.

Askofu Mkude amemwambia Rais Kikwete kuwa Shirika la Holy Ghost Missionaries ama kwa jina maarufu zaidi la Holy Ghost Fathers limeona limwalike Rais Kikwete kwenye mkutano huo kwa sababu tokea kuanzishwa kwa shirika hilo la kimataifa la The Congregation of the Holy Ghost mwaka 1703 nchini Ufaransa, hii itakuwa mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika katika Afrika.

“Hii itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa General Chapter kufanyika katika ardhi ya Afrika katika miaka 380 ya kuanzishwa kwa Shirika hili na heshima hii ya Bara la Afrika itabebwa na Jimbo la Tanzania ambalo litaandaa Mkutano huo kuanzia Juni 24 hadi Julai 22 mjini Bagamoyo,” Askofu Mkude amemwambia Rais Kikwete na kuongeza:

“Kuhusu kwa nini umechaguliwa mji wa Bagamoyo ni kwamba ilikuwa kupitia Bagamoyo ambako Shirika hilo la Kitawa liliingilia Tanganyika kwa mara ya kwanza mwaka 1868, na hivyo mji wa Bagamoyo ukawa njia ya mahubiri ya dini kuingia ndani ya Tanganyika.”

Ameongeza Askofu Mkude: “Ni heshima kubwa kwetu sisi kama taifa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kiasi hiki na wenye heshima kubwa, na kwa hakika ni heshima na imani kwa Holy Ghost Province of Tanzania, ni imani kwa Kanisa na ni imani kubwa kwa Watanzania na Rais, imani na heshima ya namna hii huambatana na wajibu mkubwa. Na kwa sababu hiyo ndiyo tumeamua kukuomba wewe kwanza kama Rais wetu na pili kama mtoto wa Bagamoyo kushiriki nasi katika tukio hili kubwa.”