RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete mwezi Oktoba, 2011 anatarajia kuzindua uwanja wa Ndege wa Mpanda wakati wa mkutano mkubwa wa uwekezaji (Investors’ Forum) wa Kanda ya Ziwa Tanganyika unaotarajia kuanza Oktoba 17.
Kauli hiyo ilitolewa jana Septemba 7, 2011 wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Rukwa na wilaya ya Mpanda mara baada ya kuwasili katika kiwanja kidogo cha ndege cha Sitalike kwenye Hifadhi ya Wanyama ya Katavi wilayani Mpanda na kupokea taarifa ya Mkoa na Wilaya.
“Mheshimiwa Rais Kikwete ndiye atakuwa mgeni rasmi wa mkutano huo na moja ya kazi atakayofanya ni kuzindua uwanja wetu wa ndege ambao utaweza kuruhusu ndege za aina mbalimbali kutua na kuleta watalii katika mbuga hii…,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza viongozi hao wa mkoa na wilaya kwamba tarehe ya mkutano huo ya Oktoba 7, 2011 iliyokuwa imetangazwa awali ilikuwa imekosewa na kwamba nia hasa ilikuwa kuhamishia mkutano huo hadi tahere 17 Oktoba.
Aliwataka wakazi wa mkoa huo kuchangamkia fursa zinazokuja kwa kuwekeza katika biashara ya hoteli na migahawa kwani kukamilika kwa uwanja huo wa ndege kutaleta changamoto ya kupata wageni wengi ambao kama maandalizi hayatafanyika mapema, watakosa sehemu nzuri za malazi na chakula.
Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika inaihusisha mikoa ya Rukwa, Kigoma na mkoa mpya wa Katavi ambayo yote mitatu imejaaliwa maliasili nyingi zikiwemo madini, vivutio vya utalii, ardhi nzuri ya kilimo na maeneo ya uvuvi.
Akizungumzia kuhusu maandalizi mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk. Rajab Rutengwe alisema washiriki zaidi ya 300 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambao utatanguliwa na wiki moja ya maonyesho ya uwekezaji kwa njia ya mabanda kuhusu fursa zilizopo kwenye wilaya za mikoa hiyo.
Dk. Rutengwe alisema mbali ya wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, baadhi ya mawaziri wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo.