Rais Kikwete kuzindua programu ya Urithi wa Ukombozi

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Na Joachim Mushi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika inayotarajiwa kufanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imetolewa leo Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi alipozungumza na wanahabri. Nchimbi amesema programu hiyo imeanzishwa ili kutambua umuhimu wa vyama vya ukombozi barani Afrika.

Aidha waziri huyo mwenye dhamana ya michezo nchini amesema uzinduzi wa programu hiyo unatokana na mchango mkubwa wa nchi zilizoshiriki ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Tanzania. “Programu itakayozinduliwa na rais itakuwa na wajibu wa kukusanya, kuweka kumbukumbu, kuhifadhi na kukumbuka nakishi ya urithi wa Afrika tangu harakati za kupigania uhuru,” alisema Waziri.

Nchimbi alizitaja nchi za awali katika kupigania uhuru na ukombozi wa Bara la Afrika kuwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana, Nigeria, Algeria, Senegali, Misiri, Swazland, na Libya huku akibainisha Tanzania ndiyo nchi iliyobuni programu husika.