Rais Kikwete kutembelea Saba Saba leo

Magari ya msafara wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye anatarajiwa kutembelea maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa viwanja vya Saba Saba Dar es Salaam.

Na Joachim Mushi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete leo anatarajia kutembelea Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Kwamujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE), Rais Kikwete atakuwa ni miongoni mwa wageni mashuhuli ambao watatembelea maonesho hayo leo kushuhudia washiriki mbalimbali wanavyoendesha shughuli zao.

Maonesho ya mwaka huu ambayo kwa kiasi kikubwa washiriki kutoka nje na ndani wameongezeka ukilinganisha na yaliopita, yamekuwa kivutio kikubwa kwa viongozi anuai na wananchi, ambao wamekuwa wakitembelea mabanda tangu ufunguzi rasmi wa maonesho hayo.

Juzi (Julai 4) jumla ya viongozi wa taifa watano kutoka Tanzania Bara na Visiwani walitembelea mabanda mbalimbali na kushuhudia taasisi za umma na binafsi, asasi anuai, washiriki binafsi pamoja na kampuni zikielezea na kuonesha shughuli wanazozifanya.

Miongoni mwa viongozi wa kitaifa ambao juzi walivutwa na kutembelea maonesho hayo ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Gharib Bilal ambaye ndiye aliyezindua maonesho hayo tangu Julai Mosi mwaka huu, Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Seif Sharif Hamad pamoja, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda pamoja na mawaziri wawili kutoka Serikali ya SMZ.

Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 8, mwaka huu baada ya kufanyika kwa siku 11 mfululizo tangu Juni 28, 2011.